Magufuli kuhutubia Kigoma mchana leo

Muktasari:

Baada ya shughuli hiyo Rais Magufuli atahutubia wakazi wa mji wa Kigoma na viunga vyake katika Kiwanja cha Lake Tanganyika mjini hapa

Kigoma. Rais John Magufuli anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji katika Manispaa ya Kigoma Ujiji leo mchana.


Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa Kigoma, mstaafu Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga amesema shughuli hiyo itafanyika saa nane mchana katika mtaa wa Katonga, kata ya Bangwe wilaya ya Kigoma mkoani hapa.

Ujenzi wa mradi huo umeanza mwaka 2013 kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani na umoja wa Ulaya (EU) kwa gharama ya uero 16 milioni, ikiwa ni zaidi ya shilingi 38 bilioni.

Mkandarasi wa mradi, kampuni ya Spencon ilishindwa kukamilisha ujenzi uliopaswa kukamilika Desemba, 2015 licha ya kuongezewa muda wa mwaka mmoja.


Licha ya kukwama huko serikali ililazimika kuongeza kipindi kingine cha mwaka mmoja ambapo sasa mradi unatarajiwa kukamilika  Desemba, 2017.

Baadhi ya sababu zilizotolewa na serikali juu ya kukwama kwa mradi ni mkandarasi kufilisika, hivyo kukosa fedha ya kugharamia ujenzi kama ilivyokusudiwa