Msako wanasa magunia 35 ya bangi

Muktasari:

Baadhi ya magunia hayo ya bangi yalikuwa mbioni kusafirishwa nchi jirani ya Kenya kwa usafiri wa pikipiki.

Tarime. Operesheni maalum dhidi ya dawa za kulevya iliyoendeshwa na Jeshi la Polisi mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya umefanikisha kukamata magunia 35 na vifurushi viwili vya bangi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Roya, Henry Mwaibambe amesema leo Februari 19 kwamba katika operesheni hiyo iliyofanyika kati ya Februari 9 hadi 17, polisi pia imekamata vifurushi 14 vya dawa ya kulevya aina ya mirungi.

Amesema katika moja ya tukio, jeshi hilo lilimnasa Joshua Nyangi mkazi wa Mtimrabu eneo la Sirari akiwa katika stendi kuu ya Tarime mjini na vifurushi 6 vya mirungi vyenye uzito wa kilo tano.

Februari 15, jeshi hilo lilinasa gari (namba za usajili zinahifadhiwa) likiwa na shehena la furushi nane za mirungi.

Katika tukio la Februari 12, polisi ilimtia mbaroni Christopher Nyangore, mkazi wa Mawasiliano mjini Tarime akiwa na magunia 11 ya bangi akijiandaa kuivusha kwenda nchi jirani ya Kenya kwa kutumia usafiri wa pikipiki.

Kamanda Mwaibambe amesema Februari 15 jeshi hilo lilimnasa Nyirabu Mwita, mkazi wa Tagota akiwa na vifurishi viwili vya bangi vyenye uzito wa kilo saba.

Februari 11 polisi ilifanikiwa kunasa magunia tisa ya bangi yakiwa yamehifadhiwa kwenye nyumba ya Keraryo Mwita mkazi wa Nkerege. Magunia hayo yalikuwa na uzito wa kilo 150.

Polisi pia pia imefanikiwa kumkamata Mwamvua Nkaina akiwa na magunia 15 ya bangi yaliyotaka kusafirishwa kwenda nchini Kenya.

Akizungumzia matukio hayo, Mkuu wa wilaya ya Tarime, Glorius Luoga amewataka wakazi wa wilaya hiyo kujiepusha na biashara haramu ili kuepuka mikono mirefu ya dola.

Mkazi wa Sirari, Mwita Marwa ameishauri Serikali kushughulikia mizizi ya kilimo na biashara ya bangi wilayani Tarime kwa kuwadhibiti wakulima ambao wanajulikana lakini hawaguswi kutokana na uwezo wao kifedha na ushawishi kwa baadhi ya viongozi.