Mahakama ilivyomwachia huru Abdul Nondo

Muktasari:

Leo Jumatatu Novemba 5, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imemwachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo baada ya kushindwa kumtia hatiani

Iringa. Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imemuachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka iliyotoa dhidi yake.

Nondo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapisha taarifa za uongo kwamba “nipo hatarini” na kuzisambaza mtandaoni na kutoa taarifa za uongo kwa askari Polisi Koplo Salim wa Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa kiwanda cha Pareto Mafinga.

 

Akitoa uamuzi huo leo Jumatatu Novemba 5, 2018 Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Liad Chamshana amesema katika kosa la kwanza upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha uongo wa maneno ya mshtakiwa na hata vielelezo ilivyotoa mahakamani hapo vilikuwa na walakini.

“Shahidi wa kwanza hadi wa sita hawakuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya kosa hilo na badala yake walitumia hisia na mashaka kutoa ushahidi wao na kushindwa kuithibitishia mahakama kwamba mshtakiwa ndiye aliyeandika maneno hayo ya uongo na maana ya maneno hayo yaliyosambazwa kwenye mitandao,” amesema.

 

Katika kosa la pili, Chamshana amesema upande wa Jamhuri ulishindwa pia kuthibitisha kosa la mshtakiwa huyo aliyekwenda katika kituo cha Polisi cha Mafinga kama mlalamikaji kabla hajageuziwa kibao na kuwa mshtakiwa.

“Hakuna ubishi kwamba Machi 7, 2018 mshtakiwa alikuwa Mafinga na alikwenda kituo cha Polisi kutoa malalamiko yake. Upande wa Jamhuri na utetezi wote wanakubali,” amesema.

Amesema cha kushangaza mashahidi wote saba wa upande wa Jamhuri walishindwa kutoa ushahidi unaonyesha namna mshtakiwa huyo alivyofika Mafinga na ule unaoonyesha kabla ya kufika Mafinga alikuwa wapi.

Kwa upande wa upelelezi wa shauri hilo, Chamshana amesema vyombo vilivyofanya upelelezi (Polisi) dhidi yake viliacha majukumu yao ya kipolisi ili viweze kuthibitisha kama kweli au sio kweli mshatakiwa alitekwa na badala yake vikamchukulia kama muhalifu.

“Kwa msingi huo upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kama mshtakiwa alitenda makosa hayo na hivyo Mahakama inamuachia huru,” alisema na kuongeza kwamba upande wa mashtaka unaweza kukata rufaa.