Mahakama ya Rufaa kuamua kesi ya Nzowa, Kova kugombea nyumba

Muktasari:

Mahakama ya Rufaa itakayoanza kikao chake Septemba 24 hadi Oktoba 2, 2018 itasikiliza rufaa ya maofisa waandamizi wa Polisi nchini wanaogombea nyumba ya Serikali iliyopo jirani na Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

Arusha. Mahakama ya Rufaa itakayoanza kikao chake Septemba 24 hadi Oktoba 2, 2018 itasikiliza rufaa ya maofisa waandamizi wa Polisi nchini wanaogombea nyumba ya Serikali iliyopo jirani na Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Bernard Mpepo akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Ijumaa Septemba 21, 2018, amesema kuwa jopo la majaji litaongozwa na Jaji Bethuel Mmilla akisaidiwa na Jaji Richard Mziray, Jaji Sivangilwa Mwangesi na Mwanaisha Kwariko.

 

Kesi hiyo namba 124/17/2017 ambayo Nzowa alikata rufaa kupinga uamuzi uliotolewa mwaka 2016 uliompa ushindi Kova,  inatarajiwa kuvuta hisia za wengi ikizingatiwa wanaogombea nyumba hiyo ni maafisa waastafu wa Serikali.

Mpepo amesema katika kikao hicho jumla ya mashauri 45 yatatolewa maamuzi, kati yao rufaa za jinai 18, maombi ya jinai mawili, rufaa za madai tano na maombi ya madai 20.

Kamanda Nzowa ndiye aliyefungua kesi hiyo akimlalamikia Kova kuuziwa nyumba ambayo (Nzowa) alikuwa akiishi wakati taratibu zilitaka mtumishi anayeishi kwenye nyumba ndiye auziwe nyumba hiyo.

Kova alikuwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoani Arusha na baadaye alihamishiwa kituo cha kazi na nafasi yake kuchukuliwa na Nzowa ambaye anadai kuwa na haki ya kununua nyumba hiyo.