Mwanamke aliyedhalilishwa akijifungua kulipwa fidia dola 25,000

Muktasari:

  •  Hukumu hiyo imejenga mazingira namna ambavyo matukio mengine yanayofanana na hilo yatakuwa yakitatuliwa katika nchi inayohaha kuimarisha mfumo wa huduma ya mama na mtoto.

Nairobi, Kenya. Mwanamke mmoja ambaye alidhalilishwa na akaachwa ajifungulie mtoto sakafuni katika hospitali ya kaunti moja nchini atakuwa na kitu cha kufuta machozi, baada ya Mahakama Kuu kuamuru alipwe fidia ya dola za Marekani 25,000.

Katika hukumu ya kihistoria iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Bungoma iliyoko magharibi mwa Kenya, jaji Abida Aroni alisema haki za msingi za mwanamke huyo aitwaye Josephine Majani zilikiukwa wakati wa kujifungua.

Mwanamke huyo alidhalilishwa miaka mitano iliyopita katika kisa ambacho kilizua lalama kutoka kwa raia na watetezi wa haki za kibinadamu baada ya kuangaziwa kwenye vyombo vya habari na mtandaoni.

Majani alisema wauguzi walimzaba vibao na walimdhalilisha mwaka 2013 na wakamwacha ajifungue mtoto huku watu wengine wakimtazama.

Mkasa wa mwanamama huyo ulinaswa kwa siri na kamera ya muuguzi mmoja aliyekuwa hospitalini hapo kwa mafunzo.

Jaji Aroni alisema haki za mwanamama huyo kupata huduma za afya zilikiukwa na utu wake ulidhalilishwa na hospitali ya kaunti ya Bungoma, umbali wa kilomita 400 kaskazini magharibi mwa jiji la Nairobi. Kutokana na hali hiyo akasema alipwe fidia ya dola za Marekani 25,000

Hukumu hiyo imejenga mazingira namna ambavyo matukio mengine yanayofanana na hilo yatakuwa yakitatuliwa katika nchi inayohaha kuimarisha mfumo wa huduma ya mama na mtoto.

Majani amefurahia uamuzi huo kwamba hatimaye haki imetendeka. Amesema fidia hiyo itamsaidia kumlea mtoto ambaye karibu ampoteze wakati wa kujifungua.

Mmoja wa wanasheria wa Majani, Martin Onyango alikiambia kipindi cha Focus on Africa cha shirika la utangazaji la BBC kwamba mteja wake "alilazimishwa kutembea peke yake hadi chumba cha kujifungulia ili likatolewe kondo la nyuma” baada ya kujifungulia sakafuni.

Alisema hukunu hiyo ni “ushindi mkubwa” kwa wanawake wa Kenya.

"Hii ni kudhihirisha kwamba huduma hizi lazima zitolewe katika ubora wa hali ya juu na zitolewe katika namna inayojali utu," alisema Onyango, mwanasheria mshauri mwandamizi wa Kituo cha Haki ya Uzazi.

Hukumu hiyo imetolewa wakati kukiwa na visa vingi vinavyohusiana na unyanyasaji ambavyo huripotiwa mara kwa mara katika hospitali za umma nchini Kenya. Hivi sasa waziri wa afya anafanya uchunguzi wa malalamiko ya wanawake kudhalilishwa kingono katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta.

Mwezi uliopita, katika hospitali hiyo hiyo, mgonjwa moja alifanyiwa operesheji ya ubongo wakati hakuwa na tatizo hilo. Madaktari walitakiwa kumfanyia operesheni mgonjwa ambaye damu ilivilia kwenye ubongo badala yake wakamfanyia aliyekuwa anahitaji dawa tu.