Mahakama yahalalisha matumizi ya Bangi Afrika Kusini

Muktasari:

Mbali ya Afrika Kusini, bangi imekuwa ikilimwa kwa wingi Lesotho na wakulima hutumia kama zao mbadala kujiingizia kipato

Pretoria.  Mahakama ya kikatiba nchini Afrika Kusini imehalalisha utumiaji wa dawa ya kulevya aina ya bangi kwa watu wazima katika maeneo faragha.

Uamuzi huo umepokelewa kwa furaha na makundi ya watu waliokuwa wakipigania kutaka ihalalishwe.

Katika uamuzi wake majaji walikubaliana kwa kauli moja kuruhusu watu wazima kutumia bangi wakiwa majumbani.

Akisoma uamuzi  huo jana Jumanne Septemba 18, 2018, naibu Jaji Mkuu wa Afrika Kusini, Raymond Zondo amesema sheria inayopiga marufuku watu wazima kutumia bangi ilikuwa kinyume cha katiba.

Hata hivyo, hadi sasa Serikali ya Afrika Kusini haijatoa tamko lolote kuhusiana na uamuzi huo ambao unaandika historia mpya katika Taifa hilo.

"Siyo hatia kwa mtu mzima kutumia au kugusa bangi akiwa katika eneo la faragha hasa ikiwa anafanya hivyo kwa matumizi yake ya kibinafsi,” amesema.

Baraza la ukuzaji bangi nchini Afrika Kusini limeunga mkono uamuzi wa mahakama na kutoa wito kwa Serikali kuwaondolea mashtaka watu waliokutwa na bangi.

Mbali ya Mahakama ya Afrika Kusini kuhalalisha matumizi hayo, matumizi ya bangi nchini Lesotho yanaruhusiwa, ikielezwa kuwa ni dawa.

Bangi imekuwa ikilimwa nchini humo  na sehemu kubwa husafirishwa nje ya nchi ikiwamo Afrika Kusini.

Wakulima nchini Lesotho wanalima bangi kwa ajili ya matumizi yao nyumbani na kusafirisha nje ya mipaka kutokana na hali ya umasikini waliyonayo.