Mahakama yakataa wanandoa kugawana mali nusu kwa nusu

Muktasari:

Jaji wa Mahakama Kuu John Mativo amesema kuwa Sheria ya Mali ya Ndoa (MPA) ya mwaka 2013, ambayo husema wanawake watagawana mali na familia kulingana na michango yao binafsi endapo watatalikiana, ni ya kikatiba na kisheria.

Nairobi, Kenya. Wanandoa wachapakazi waliibuka washindi Jumatatu katika vita kali vya kisheria baada ya mahakama kuimarisha ulinzi wa mali waliyochuma dhidi ya wenzao wanaoingia katika ndoa wakiwa na lengo la kuchuma mali ambayo wala hawakushiriki kuitafuta.

Jaji wa Mahakama Kuu John Mativo amesema kuwa Sheria ya Mali ya Ndoa (MPA) ya mwaka 2013, ambayo husema wanawake watagawana mali na familia kulingana na michango yao binafsi endapo watatalikiana, ni ya kikatiba na kisheria.

Hukumu hiyo imetolewa baada ya Shirikisho la Wanasheria wa Wanawake (Fida) kutaka kifungu cha 6 (3) cha Sheria hiyo kitangazwe kuwa kinyume cha sheria kwa sababu kinasema kwamba, ikiwa watatalikiana, mali ya wanandoa inapaswa kugawanywa kati ya wanandoa kulingana na mchango wao kwa upatikanaji wake.

Fida ilikuwa inataka wanandoa kugawanya mali sawa, lakini Jaji Mativo alisema kuwa hii itafungua mlango kwa watu kuingia katika ndoa na kutoka ikiwa watatalikiana akiwa na mali zaidi ya anayostahili.

"Kwa kusema kwamba kila upande utapata haki yake kulingana mchango wake, sehemu inazingatia kanuni ya usawa katika ndoa," alisema Justice Mativo.