Mahakama yaliteua Gazeti la Mwananchi kuwatafuta wadaiwa

Muktasari:

Wanakabliwa na madai ya uvamizi na uporaji wa ardhi wilayani Mkuranga

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imeliteua Gazeti la Mwananchi kuwatafuta wadaiwa katika kesi ya uporaji ardhi Kata ya Tambani wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani ili wahudhurie mahakamani.

Uamuzi huo ulitolewa juzi na Jaji Rehema Mkuye kesi hiyo ilipotajwa kutokana na wadai kueleza wameshindwa kuwafikishia wadaiwa wengine wito wa kuhudhuria mahakamani kwa kuhofia usalama wao.

Kesi hiyo namba 85 ya 2016 imefunguliwa na wakazi wa Kijiji cha Tambani, Haruna Mbonde na wenzake 18 dhidi ya kikundi cha watu 38 wanaodaiwa kuwa wavamizi wa ardhi na mali zao.

Kesi hiyo ilipotajwa juzi, wadaiwa hawakufika mahakamani na wakili wa wadai, Hussein Hitu alidai wengine wamekamatwa na wako mahabusu, hivyo wasingeweza kufika kwa kuwa hapakuwa na hati ya kuwatoa mahabusu.

Hitu alidai wadaiwa wengine waliopo eneo la mgogoro hawajafikishiwa hati za wito wa kufika mahakamani kwa kuwa hakuna usalama na Serikali ya Mtaa imeshindwa kuzipeleka.

Aliiomba mahakama itoe amri wadaiwa hao watangazwe kwenye vyombo vya habari ili wafike mahakamani tarehe itakayopangwa kutajwa shauri hilo.

Jaji Mkuye alitoa amri upande wa wadai utoe tangazo kwenye Gazeti la Mwananchi kuwataka wadaiwa kuhudhuria mahakamani Oktoba 30, kesi hiyo itakapotajwa.

Wadaiwa Shaban Kapelele na wenzake 37 wanadaiwa kuvamia ardhi na kupora mali za wadai zikiwamo nyumba na mazao. Pia wanadaiwa kuwapiga na kuwajeruhi wadaiwa kwa kutumia silaha za jadi na kusababishia vifo wengine.

Kwenye hati ya madai imeelezwa wadaiwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani baada ya uvamizi na kupora ardhi huwauzia watu wengine.