Mahakama yampiga chini AG Burundi, Bunge ‘lanunua kesi’

Muktasari:

  • Msingi wa hoja ya mwanasheria huyo wa Burundi, uliegemea kutozingatiwa kanuni za kudumu za bunge ikiwamo akidi kutokana na wabunge wa Burundi kutoshiriki uchaguzi huo.

Arusha. Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) imetupilia mbali maombi ya mwanasheria mkuu wa Burundi (AG), aliyetaka kusitisha shughuli za Bunge la jumuiya hiyo (Eala) na Spika Martin Ngoga hadi kesi ya msingi itakapokuwa imeamriwa.

Msingi wa hoja ya mwanasheria huyo wa Burundi, uliegemea kutozingatiwa kanuni za kudumu za bunge ikiwamo akidi kutokana na wabunge wa Burundi kutoshiriki uchaguzi huo.

Uchaguzi wa Spika wa Eala uliofanyika Desemba 19 mwaka jana, ulimchagua Ngoga kutoka Rwanda umeendelea kutikisa nchi wanachama kutokana na kile kinachoelezwa huenda ukaathiri mtangamano wa jumuiya.

Katika uamuzi mdogo uliotolewa kwenye mahakama hiyo kitengo cha awali juzi, jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Monica Mugenyi, Fakihi Jundu na Isaac Lenaola walisema maombi yake yamepitwa na wakati kwa sababu Spika Ngoga tayari ameapishwa na kuanza kazi.

Hata hivyo, Jaji Mugenyi alikubali kuwa kuna hoja ya msingi ya kubishaniwa ambayo ni uhalali wa uchaguzi wenyewe, ambao mlalamikaji anadai pamoja na mambo mengine akidi ya kufanya kikao kilichomchagua Spika haikutimia.

Katika uchaguzi huo wabunge wote tisa wa Burundi na saba wa Tanzania walisusia kikao hicho, wakidai utaratibu wa kumpata mgombea wa nafasi ya uspika haukufuatwa huku nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi zikisimamisha wagombea.

“Mahakama imetupilia mbali maombi hayo na imeagiza kesi ya msingi inayopinga mchakato mzima wa uchaguzi wa Spika wa bunge, isikilizwe na kutolewa uamuzi,” alisema Jaji Mugenyi.

Kabla ya uamuzi huo, mahakama ilizuia maombi yaliyowasilishwa na mbunge wa Eala kutoka Uganda, Fred Mbidde aliyetaka kufanyike marekebisho ili awe mmoja wa watu wenye maslahi na kesi hiyo kwa lengo la kupinga maombi ya AG Burundi.

Pia, mahakama ilimkatalia mpeleka maombi ya kutaka kuunganishwa kwenye kesi hiyo kama rafiki wa mahakama. Awali aliomba kuunganishwa kama rafiki wa mahakama, baadaye alibadilisha ili aunganishwe kwa sababu ana maslahi ni mbunge wa Eala kisha kuondoa ombi lake.

Katika tukio jingine, kikao cha dharura kilichofanyika jana, Eala kwa kauli moja limepitisha muswada kwa kupiga kura ya kuwa sehemu ya kesi namba 2 ya mwaka 2018 iliyofunguliwa na mwanasheria mkuu wa Burundi dhidi ya katibu mkuu wa EAC.

Baada ya mbunge kutoka Uganda, Fred Mbidde kuwasilisha muswada wake na Spika Ngoga kuruhusu wabunge kuchangia, mbunge Chris Opoka aliomba Bunge kusitisha kifungu cha kanuni za kudumu za bunge kifungu 12(d) kinachohusu akidi ili kuruhusu wabunge kujadili.

Wakati kikao kinaanza wabunge wawili pekee wa Burundi kati ya tisa, ndio waliokuwa ukumbini, huku kanuni ikitaka angalau kikao kiendelee wanahitajika wabunge watano kutoka kila nchi.