Friday, November 10, 2017

CUF yazuiwa kuwavua uanachama ‘wabunge’ wanane

 

By James Magai, Mwananchi jmagai@mwananchipapers.co.tz

 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekizuia Chama cha Wananchi (CUF) kujadili na kuwafukuza uanachama waliokuwa wabunge wanane wa Viti Maalumu na madiwani wawili.
Hata hivyo, Mahakama imetoa uamuzi huo huku tayari chama hicho kikiwa kimeshawavua uanachama na baadaye kupoteza nafasi zao za ubunge na udiwani.
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Novemba 10,2017 na Jaji Lugano Mwandambo kutokana na maombi yaliyofunguliwa na Miza Bakari Haji na wenzake saba waliokuwa wabunge wa viti maalumu na madiwani wawili wa viti maalumu, ambao pia walivuliwa uanachama.
Zuio hilo la mahakama linaihusu Bodi ya CUF, Mwenyekiti wake wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya, ambao walikuwa ni miongoni mwa wajibu maombi, ambao pia ni wadaiwa katika kesi ya msingi.
Hata hivyo, wakati ikitoa zuio hilo, Mahakama imenawa mikono dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo pia ilikuwa ni miongoni mwa wajibu maombi, kuwa haina mamlaka ya kuchunguza uamuzi wake.
Pia, Mahakama ilitupilia mbali madai dhidi wakurugenzi wa manispaa za Ubungo na Temeke, ambao nao walikuwa ni wajibu maombi hayo.
Katika maombi hayo, waombaji walikuwa wakiiomba Mahakama kutoa amri ya zuio la muda dhidi ya Bunge kutokuwaapisha wabunge wapya walioteuliwa na NEC badala ya walalamikaji.
Pia, waliiomba Mahakama itoe amri ya zuio la muda dhidi ya wakurugenzi wa manispaa za Ubungo na Temeke kutokuwateua madiwani wengine badala yao na kuwaapisha, kusubiri kumalizika kwa kesi yao ya msingi waliyoifungua wakipinga kuvuliwa uanachama.
Hata hivyo, Agosti 25 Mahakama ilitupilia mbali  maombi ya zuio dhidi ya Bunge kutokuwaapisha wabunge walioteuliwa kuchukua nafasi zao baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
 Wadai wengine ambao walikuwa wabunge wa Viti Maalumu  ni Savelina Silvanus Mwijage, Salma Mohamed Mwassa, Raisa Abdallah Musa na Riziki Shahari Mngwali.
Wengine katika nafasi ya ubunge ni Hadija Salum Al- Qassmay, Halima Ali Mohamed na Saumu Heri Sakala wakati madiwani ni Elizabeth Alatanga Magwaja na Layla Hussein Madib.

-->