Maisha mapya uraiani kwa waliopata msamaha pasua kichwa

Muktasari:

Rais alitoa msamaha huo ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa sherehe za uhuru wa Tanganyika ambao sasa umetimiza miaka 56.

 Nguza Vicking na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ wanaweza kuonja maisha mapya mazuri baada ya kutoka gerezani juzi, lakini tatizo ni wafungwa wengine zaidi ya 8,000 waliopata msamaha wa Rais John Magufuli, juzi.

Rais alitoa msamaha huo ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa sherehe za uhuru wa Tanganyika ambao sasa umetimiza miaka 56.

Wako waliokuwa wanatembelewa na ndugu na wako ambao hawajui ndugu zao kama bado wako hai, wako eneo walilowaacha au kama shughuli zao binafsi za kujiingizia kipato zipo.

Lakini kwa kutumia kipaji chao cha muziki na umaarufu wao, Nguza na Papi Kocha wanaweza kuwa na uhakika wa maisha mapya; wanasubiriwa kwa hamu na bendi, mameneja wa wanamuziki, waandaaji wa matamasha, wanamuziki na hata makanisa.

Na tayari wimbo walioimba wawili hao wa “Seya” umeshaanza kuchezwa redioni na kwenye mitandao ya kijamii.

Na kuthibitisha umaarufu wao, vyombo vya habari na mamia ya wananchi walijitokeza kuwalaki wawili hao walipokuwa wakiungana na familia yao, ndugu jamaa na marafiki juzi.

Kwa picha zilizosambazwa juzi na jana baada ya kuachiwa kwao, wawili hao walionekana kubadilika. Walikuwa nadhifu wanaoweza kualikwa popote na walipokelewa na watu maarufu na kukaribishwa uraiani.

Babu Seya na mwanaye si pekee kwenye orodha ya waliopata msamaha wa Rais kati ya wafungwa 666 waliohukumiwa kifungo cha maisha. Wamo pia 61 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa. Hao ni miongoni mwa 522 waliokuwa wanasubiri kutekelezwa kwa adhabu hiyo.

Kwa jumla, Rais Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 8,157 wakiwamo 1,828 walioachiwa huru na 6,329 waliopunguziwa adhabu. Jana, taarifa ya Ikulu ilisema Rais Magufuli ameshasaini nyaraka za msamaha huo.

Msamaha wa Rais unapunguza msongamano uliopo kwenye magereza yote nchini ambao kabla ya uamuzi wake, Rais alisema kulikuwa na wafungwa 39,000.

Wanarudije uraiani?

Wakati ratiba ya shughuli ya Nguza na mwanaye imejaa, hali ya sintofahamu imetawala kwa wengine waliopotezana nao kwa zaidi ya miaka 10 ya kukaa gerezani.

Wakati anatangaza msamaha, Rais Magufuli alisema kuna watu wametumikia kifungo kwa muda mrefu, akitoa mfano wa mtu aliyefungwa akiwa na miaka 18 na sasa hivi ana zaidi ya miaka 60.

“Anaitwa Mganga Matonya, ana miaka 85 na ameshakaa gerezani miaka 37 baada ya kuhukumiwa ukiacha saba ya kusubiri hukumu. Jumla amekaa miaka 44,” alisema Rais.

Watu wa aina ya Matonya ni wengi ambao wakirudi mtaani wanaweza wasikumbuke chochote katika nchi ambayo miji inakua kwa kasi, huku waliokuwa vijana wenzao huenda hawapo tena duniani na kama wapo ni vikongwe.

Pia hawatawakuta viongozi wa Serikali za mitaa waliowaacha.

Mkuu wa magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Augustine Mboje anasema wafungwa wanaostahili msamaha hutoka kama walivyoingia na kurudishwa walipokuwa wanaishi. “Kama wametoka mbali, husafirishwa mpaka kijijini kwao. Waliopo mjini, huwasiliana na ndugu zao. Hakuna wanachopewa kwa ajili ya kwenda kuanzia maisha mapya,” alisema kamishna huyo.

Kwa wanaoachiwa bila kuwa na uhakika wa waendako, hali yao ni mbaya zaidi.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo-Bisimba anasema endapo tathmini ya kina haitafanywa, msamaha huu unaweza kuharakisha kifo chao.

“Yupo kijana mmoja ambaye baada ya kukaa gerezani kwa miaka 17, alishinda rufaa yake na akaachiwa. Aliporudi uraiani akakuta mambo mengi yamebadilika. Ndugu zake wamehama na hana pa kwenda. Alikuja ofisini kwetu na kutuambia atakaa hapo akisubiri kifo chake,” alisema Dk Bisimba.

Washiriki shughuli za kiuchumi

Kutokana na baadhi yao kushindwa kumudu maisha ya uraiani baada ya kutumikia vifungo vyao, Kamishna Mboje anasema Jeshi la Magereza limependekeza uandaliwe utaratibu utakaowawezesha wafungwa kushiriki shughuli za kiuchumi na kujipatia kipato.

“Watakaokuwa wanashiriki shughuli hizo watatunziwa fedha ambazo zitatokana na shughuli hizo ili ziwasaidie wakitoka. Baadhi ya mataifa yamefanikiwa kwenye hili. Serikali ikiridhia, sisi pia tutakuwa na utaratibu huo,” alisema.

Alisema zamani, kuna baadhi ya wafungwa walikuwa wanakataa kutoka gerezani hata baada ya kumaliza kutumikia vifungo vyao au kupewa msamaha wa Rais.

Licha ya kutunziwa fedha kama jeshi hilo linavyopendekeza, Dk Bisimba alisema maisha ya uraiani yana changamoto nyingi hivyo utaratibu ubadilishwe na wafungwa wawe wanajengewa uwezo wa kijasiriamali.

Alitoa mfano kwa watumishi walioajiriwa serikalini au katika kampuni binafsi ambao hupoteza maisha muda mfupi baada ya kustaafu.

“Zamani walikuwa wanapewa mafunzo na vitendea kazi. Wakija uraiani wanajiajiri,” alisema.