Maisha ya Lulu ndani ya saa 512 za kifungo cha nje

Muktasari:

  • Novemba 13, mwaka jana Elizabeth maarufu kwa jina la Lulu alianza maisha ndani ya Gereza la Segerea na alitarajiwa kumaliza adhabu yake Machi 12, mwakani. Hata hivyo, bahati ni kama ilikuwa upande wake kwani katika maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano Aprili 26, Rais John Magufuli alitoa msamaha wa kupunguza robo ya adhabu kwa baadhi ya wafungwa, naye akawa miongoni mwa wanufaika.

Mwigizaji Elizabeth Michael alihitimisha maisha ya jela Jumamosi iliyopita baada ya kukaa gerezani kwa siku 186, lakini bado ni mfungwa ambaye anaendelea kutumikia adhabu yake akiwa na siku 184 mbele yake zitakazoambatana na kazi za kijamii.

Novemba 13, mwaka jana Elizabeth maarufu kwa jina la Lulu alianza maisha ndani ya Gereza la Segerea na alitarajiwa kumaliza adhabu yake Machi 12, mwakani. Hata hivyo, bahati ni kama ilikuwa upande wake kwani katika maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano Aprili 26, Rais John Magufuli alitoa msamaha wa kupunguza robo ya adhabu kwa baadhi ya wafungwa, naye akawa miongoni mwa wanufaika.

Msamaha huo ulimpunguzia adhabu akitakiwa kutoka Novemba 12, mwaka huu, lakini kwa sasa mwigizaji huyo aliyepatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia nyota mwenzake wa filamu Steven Kanumba, atatumikia adhabu mbadala ya nje na si kifungo.

Hata hivyo, baada ya maisha ya jela, Lulu anakabiliwa na maisha mengine mapya ya kifungo cha nje yakiambatana na saa nne za kufanya kazi za jamii kila siku, isipokuwa siku za mapumziko kwa maana ya Jumamosi, Jumapili pamoja na sikukuu, ambazo ni jumla ya saa 512.

Katika siku 184 zilizosalia kufikia Novemba 12 ambapo atamaliza kifungo cha nje, Lulu atafanya kazi hiyo kwa siku 128 ambazo ni sawa na saa 512. Siku hizo hazihusishi Jumamosi 27, Jumapili 26 na sikukuu za Idd el Fitri, Nane Nane na Idd el-Adha ambazo jumla ni siku nne.

Adhabu yake mpya

Akizungumzia adhabu mpya ya msanii huyo, mkurugenzi wa Probesheni na Huduma za Jamii, Charles Nsaze alisema jana kuwa Lulu ameanza kuitumikia tangu alipotoka gerezani Mei 14 kwa kufanya usafi katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi zilizopo eneo la Posta jijini Dar es Salaam .

Alisema kila siku mwigizaji huyo atatumia saa nne kusafisha mazingira kisha ataendelea na shughuli zake nyingine za ujenzi wa Taifa.

“Atapumzika siku za Jumamosi na Jumapili au siku za sikukuu. Hatakuwa peke yake kwa kuwa tayari hapa wapo wafungwa wengine tisa wanaofanya kazi za usafi wa mazingira,” alisema Nsaze.

Alipoulizwa iwapo Lulu atatakiwa kuvaa sare awapo katika kazi hiyo, mkurugenzi huyo alisema msanii huyo pamoja na wafungwa wengine wa kifungo cha nje wanaotumikia adhabu hawapangiwi namna ya uvaaji.

Maisha ya uigizaji, biashara

Akizungumzia iwapo msanii huyo anaweza kuendelea na maisha ya uigizaji na biashara zake, Nsaze alisema hilo ndilo lengo la kuwatoa wafungwa hao ili washiriki katika ujenzi wa Taifa kwa kufanya shughuli mbalimbali.

Alisema Dar es Salaam pekee kuna wafungwa wanaotumikia kifungo cha nje zaidi ya 1,000 ambao wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, isipokuwa wanapaswa kufuata masharti waliyowekewa ikiwamo kushiriki katika kazi walizopagiwa kila siku.

Nsaze anasema Lulu anaweza kuolewa, kucheza filamu, kushiriki katika utengenezaji wa matangazo au kuingia ubia wowote wa kibiashara.

“Lulu anaweza hata kuamua kubeba ujauzito, lakini kama utamfanya ashindwe kufanya kazi zake ina maana atakuja kuzifidia saa zake za kazi akijifungua ili akamilishe kifungo chake lakini hatumzuii chochote,” alisisitiza.

Mahojiano hapana

Mkurugenzi huyo alisema suala jingine analobanwa nalo Lulu kwa sasa ni kushiriki mahojiano na chombo chochote cha habari, akisema hilo ni mpaka apewe kibali na mkurugenzi anayemsimamia wizarani hapo.

“Inategemea anataka kuzungumza nini, hapo sasa mpaka mkurugenzi aridhie anaweza kumruhusu akiona inafaa,” alisema.

Pia asipatwe na kosa

Suala jingine analopaswa kukaa nalo mbali ni lolote lile linaloweza kumsababishia kutenda vitendo visivyokubalika mbele ya jamii kama vile ugomvi.

Iwapo atafanya kosa lolote katika kipindi hiki, Nsaze anasema wataangalia uzito na kwa mara ya kwanza anaweza kupewa onyo la mdomo au maandishi, na iwapo ataonekana kutojirekebisha atafunguliwa mashtaka na ikibidi kurudishwa gerezani.

Haki na wajibu kisheria

Akizungumzia Sheria ya Huduma za Jamii namba 6 ya mwaka 2002, wakili wa kujitegemea, Reuben Simwanza alisema inaainisha haki na wajibu wa mfungwa wa nje ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za makazi hasa anapohama kutoka eneo moja kwenda jingine.