Maiti iliyozikwa kwa kukosa ndugu yatambulika Ukerewe

Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima (kushoto) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jonister  Mhagama, viongozi na maofisa wengine wa Serikali wakihakiki makaburi ya waliozikwa bila kutambuliwa ili kubaini kaburi la Muleba Mavere ambaye mume wake Matindi Mavere na ndugu zake wengine wamejitokeza.

Muktasari:

  • Mmoja kati ya watu wanne waliozikwa katika mazishi ya kitaifa ya waliokufa katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere ametambulliwa baada ya ndugu zake kujitokeza na vipimo vyao vya vinasaba (DNA) kufanana na vya marehemu


Ukara. Mtu mmoja kati ya wanne waliozikwa jana Septemba 23 bila kutambulika, ametambuliwa baada ya ndugu zake kujitokeza na vipimo vyao vya vinasaba kufanana.

Aliyetambuliwa ni marehemu Muleba Mavere ambaye awali alizikwa kwa utanbulisho wa namba 10 K.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kukabidhi kaburi la marehemu kwa ndugu zake kwa ajili ya ibada na taratibu za kifamilia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu), Jenister Mhagama amesema vipimo vya kitaalam vimethibitisha bila shaka kuwa vinasaba vya marehemu vimelingana na mmoja wa watoto wake wa kike.

"Tumefanya vikao na familia hadi jana usiku ambapo baada ya kuridhika na maelezo yao, wataalam walikamilisha kwa kufanya vipimo ambavyo vimetupa uhakika," amesema Mhagama

Kutambuliwa kwa marehemu Muleba kunafanya waliozikwa bila kutambulika kubakia watatu.

Miongoni mwa ndugu marehemu waliojitokeza ni pamoja na mume wake, Matindi Mavere mkazi wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera na watoto wake wawili.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ambaye yuko Ukara kusaidiana na mwenzake John Mongella kuratibu kazi ya uokoaji amewataka watu wenye uhakika kuwa ndugu zao walikuwa ndani ya kivuko cha Mv Nyerere lakini hawajaonekana kujitokeza.

"Hatutafanya makosa katika utambuzi; tutawahitaji na kijiridhisha na kukamilisha utambuzi kwa vipimo ya DNA," amesema Malima

Mazishi ya kitaifa ya watu tisa, wanne wakiwa ambao hawakutambulika na watano waliotambuliwa lakini ndugu wakakubali wazikwe kwenye makaburi ya pamoja yalifanyika katika makaburi yaliyochimbwa hatua 250 kutoka gati la Bwisya ambako shughuli za uokoaji zinaendelea.

Soma Zaidi: