Maiti yaokotwa vichakani Picha ya Ndege

Diwani wa Kata ya Picha yandege Robart Machumbe kulia akiwa na baadhi ya Wakazi wa Mtaa wa Lulanzi Kata ya Picha ya Ndege Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoani Pwani wakiwa kwenye eneo ambalo ilikutwa maiti ya mtu ambaye hajatambulika jina wala sehemu anakotoka ambapo pia ulikuwa na jeraha usoni na kidevuni huku pembezoni kukiwa na ganda la risasi ambapo eneo hilo ni miongoni mwa mashamba pori ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu. Picha na Sanjito Msafiri

Muktasari:

Mwili wa mwanamume huyo uliokotwa huku pembeni mwake kukiwa na ganda la risasi ya bunduki.

Pwani. Mwanamume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 ameuawa na watu wasiofahamika kisha mwili wake kutupwa kwenye vichaka katika mtaa wa Lulanzi, Kata ya Picha ya Ndege mkoani Pwani.

Mwili wa mwanamume huyo uliokotwa huku pembeni mwake kukiwa na ganda la risasi ya bunduki.
Mbali na ganda hilo, maiti hiyo ilikuwa na jeraha kwenye paji la uso pia zimekutwa nyaraka mbalimbali vikiwemo vitambulisho, ramani ya nyumba na begi lililokuwa limewekwa vitu hivyo.

Vitu hivyo vinadaiwa ni mali ya mkazi wa Picha ya Mdege (jina linahifadhiwa) ambaye inadaiwa aliporwa na majambazi baada ya kujeruhiwa kwa risasi siku hivi karibuni.
Mkazi huyo alivamiwa wakati alipokwenda kufanya malipo kwa mafundi ujenzi waliokuwa wakimjengea nyumba katika kata hiyo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Lulanzi, Thobiasi Shilole amesema taarifa za kuwapo maiti hiyo ikiwa imeharibika alizipata juzi usiku kutoka kwa wananchi walioiona wakiwa wanapita.

Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani, Boniventura Mushongi alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kuwa mwili huo ulikutwa na jeraha dogo chini ya kidevu na jingine kubwa utosini na mwili ukiwa umeanza kuharibika. Pembezoni mwake kulikutwa na mask, kofia ya kuficha sura na ganda la la risasi ya SMG na kusema kuwa mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha.
"Pia tulikuta nyaraka mbalimbali ambazo miongoni mwa hizo ni pamoja na ramani za nyumba stakabadhi za kibali cha ujenzi  vyote vikiwa na majina ya Beno Nyoni ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Picha ya Ndege aliyefanyiwa tukio la unyanganyi wa kutumia silaha hivi karibuni na kujeruhiwa ambaye hivi sasa anaendelea na matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili na sisi tunaendelea na uchunguzi zaidi," alisema