Majahazi yenye bidhaa za magendo yakamatwa

Muktasari:

  • Meneja wa Forodha TRA, Edward Ndupa alisema bidhaa hizo zilizokamatwa hivi karibuni zikiwa ndani ya majahazi hayo ni sukari tani tano, vitenge, khanga na mafuta ya kupikia madumu 470 ya lita 20 kila moja vyote vikiwa na thamani ya Sh35 milioni 35.

Tanga. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamekamata majahazi manne yenye bidhaa mbalimbali katika Kijiji cha Kigombe Wilaya ya Muheza mkoani hapa yaliyokuwa yakipita njia za panya yakitokea visiwani Zanzibar.

Meneja wa Forodha TRA, Edward Ndupa alisema bidhaa hizo zilizokamatwa hivi karibuni zikiwa ndani ya majahazi hayo ni sukari tani tano, vitenge, khanga na mafuta ya kupikia madumu 470 ya lita 20 kila moja vyote vikiwa na thamani ya Sh35 milioni 35.

Ndupa alifafanua kuwa hadi sasa wafanyabiashara wenye bidhaa hizo hawajafahamika hivyo, mamlaka inafanya utaratibu wa kuzitaifisha moja kwa moja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Edward Bukombe aliwataka wafanyabiashara wote wanaojihusisha na biashara za magendo kuacha vitendo hivyo na kuongeza kuwa wataendelea kushirikiana na TRA kwa ajili ya kuwakamata wanaosafirisha bidhaa kupitia njia sizizo rasmi.

“Natoa wito kwa wafanyabiashara wote wanaokwepa kulipa kodi na kupitisha bidhaa zao katika njia za magendo kuacha mara moja tabia hiyo. Polisi tumejipanga vizuri na tutaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuwabaini na kuwakamata wafanyabiashara wanaokiuka sheria ikiwa ni pamoja na kukamata bidhaa husika,” alisema Bukombe.

Pia, aliwahimiza wafanyabiashara kufuata sheria, kanuni na taratibu ili waweze kufanya biashara zao bila kubughudhiwa na hatimaye wajiingizie kipato halali.