Majaji wastaafu kuapishwa kuwa mawakili kwazua jambo

Baadhi ya mawakili wakiwa kwenye sherehe ya kuapishwa mawakili wapya 549 jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame


Muktasari:

Yaelezwa kuwa mtu akishastaafu ujaji hawezi kusimama tena Mahakama

Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume amefafanua usajili wa majaji wastaafu kuwa mawakili akisema hawataweza kusimama mbele ya Mahakama kama mawakili wengine.

Jana, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma aliwakubali na kuwasajili mawakili wapya 549 wakiwamo majaji wastaafu wanne ambao ni Edward Rutakangwa, Sekieti Kihio, John Ruhangisa na Ibrahim Mipawa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Fatma alisema majaji hao wastaafu wanaweza kufanya kazi nyingine za usuluhishi ambazo hazitawahitaji kusimama mbele ya Mahakama.

“Sisi tunafuata mfumo wa Mahakama wa Waingereza ambao una utaratibu kwamba mtu akishastaafu ujaji hawezi kusimama tena mbele ya Mahakama au kufanya kazi ya uwakili,” alisema.

Kiongozi huyo wa TLS alifafanua kuwa, majaji waliosajiliwa kuwa mawakili waliteuliwa nafasi hiyo kupitia njia nyingine tofauti na uwakili. Hata hivyo, alibainisha kwamba sasa wamekuwa mawakili wa heshima.

“Kwa kawaida majaji wanateuliwa kutoka kwenye makundi matatu; kwanza, ni wale waliokuwa mawakili, pili ni wanasheria wa serikali; na tatu ni mahakimu ambao walikuwa kwenye mfumo wa Mahakama na kupandishwa cheo mpaka ngazi ya jaji,” alifafanua.

Fatma aliongeza kuwa majaji wastaafu waliosajiliwa hawakuwahi kuwa mawakili, hivyo wamekamilisha dhamira zao na kuwa mawakili wanaotambulika kisheria.

Awali, wakati wa hafla hiyo, Jaji Mkuu, Profesa Juma aliwataka mawakili hao wapya kwenda kutoa huduma vijijini na kuangalia bei zao ili kuwawezesha wananchi kupata huduma yao.

“Changamoto imekuwa ni mawakili wengi kujazana mijini, wakati hata huko vijijini wananchi wanawahitaji. Natoa wito kwao kwenda kufanya kazi vijijini na kuweka bei ambazo wananchi wanazimudu,” alisema Jaji Mkuu.

Kiongozi huyo wa Mahakama nchini alibainisha kwamba idadi ya mawakili imeongezeka mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana ambao ulikuwa na wahitimu 340.

Wakili mpya, Haman John alisema atakwenda kuwatetea wananchi na kuhakikisha kwamba wanapata haki zao.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Gazeti la Mwananchi hivi karibu, Jaji mstaafu Thomas Mihayo alisema endapo jaji atasimama kama wakili, haweza kumshawishi hakimu akaona kile anachosema ndicho sahihi. “Kwa mtazamo wangu naona hii siyo sahihi, ingawa kuna majaji kadhaa wana ‘practice’ kama mawakili,” alisema.