Majaliwa: Uhuru wa watu kujieleza Tanzania umejaa

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa ameihakikishia jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania watu wana uhuru mkubwa wa kujieleza na kupata habari.
  • Jana Jumatano Oktoba 24, 2018, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amehudhuria maadhimisho ya miaka 73 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN) ambapo ametumia siku hiyo kutoa ujumbe kwa vijana 

 


Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa ameihakikishia jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania hakuna ubanaji wa vyombo vya habari wala taasisi zisizo za kiserikali.

Pia amesisitiza kuwa watu wana uhuru mkubwa wa kujieleza na kupata habari.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 73 ya Umoja wa Mataifa (UN), iliyohudhuriwa na viongozi wa mashirika mbalimbali yaliyo chini ya umoja huo, mabalozi na mratibu mkazi wa UN nchini, Alvaro Rodriguez.

“Tunapenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Tanzania inaongozwa na Katiba na sheria za nchi zinazotoa uhuru wa kujieleza na kupata habari. Hii inadhihirishwa na uwepo wa jumla ya vituo vya redio 152, ambavyo kati ya hivyo vitatu vinamilikiwa na Serikali,” alisema Waziri Mkuu.

Hata hivyo, alisema mtu yeyote akienda kinyume na sheria, Serikali inamwajibisha kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu imekuja wakati ambao kumekuwepo na malalamiko kutoka vyama vya upinzani na asasi za kiraia kuwa kuna ukandamizaji wa haki ya kujieleza na kutoa maoni.

Malalamiko ya kubanwa kujielezea yamekuwa yakitolewa na watu wa makundi mbalimbali wakiwemo wanaharakati, wananchi wa kawaida, wanasiasa, viongozi wa dini na pia wanahabari.

Mei 18, aliyekuwa askofu wa Kanisa la Anglikana, Dk Valentino Mokiwa aliiambia Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW) kuwa yeye ni miongoni mwa waathirika wa uminywaji wa haki ya kujieleza na amekuwa akiishi kama mtu wa daraja la nne.

Septemba 26, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga wakati wa sherehe za miaka 20 ya kituo hicho, alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani kumekuwepo na hofu ya watu kujieleza na wanaojaribu kupaza sauti wanachunguzwa uraia na ulipaji wao wa kodi.

Jana katika hotuba yake, pia Majaliwa alitoa ufafanuzi wa shutuma dhidi ya Serikali kutoka kwa baadhi ya jumuiya za kimataifa kuhusu kuwarudisha kwao wakimbizi wa Burundi akisisitiza kuwa hiyo ni hiari na wanatekeleza suala hilo baada ya kujiridhisha kuwa amani na usalama vimerejea nchini humo.

Tangu Septemba 2017, Tanzania kwa kushirikiana na Burundi pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi (UNHCR) wamekuwa wakiwarejesha kwa hiari wakimbizi kutoka nchi hiyo.

“Katika sera na sheria zetu imesisitizwa kuwa nchi yetu itawahifadhi wakimbizi kwa kipindi ambacho nchi zao zina matatizo ya usalama na amani na hawawezi kurejea, (ila) pale hali ya usalama inapoimarika wanapaswa kurejea kwao,” alisema Waziri Mkuu.