Majaliwa apiga marufuku mishumaa bwenini

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku matumizi ya viberiti, mishumaa na ‘hita’ za kuchemshia maji kwa wanafunzi wa bweni ili kuepusha majanga ya moto.

Muktasari:

  • “Kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza vifaa vya kienyeji vya kuchemsha maji mabwenini jambo hili ni la hatari, kwani linaweza kusababisha ajali ya moto, hivyo ni marukufu kwa mwanafunzi kutumia vifaa hivyo,” amesema.

Lindi. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku matumizi ya viberiti, mishumaa na ‘hita’ za kuchemshia maji kwa wanafunzi wa bweni ili kuepusha majanga ya moto na atakayekutwa atachukuliwa hatua kali.

“Kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi hasa wa masomo ya fizikia kutengeneza vifaa vya kienyeji vya kuchemsha maji mabwenini jambo hili ni la hatari, kwani linaweza kusababisha ajali ya moto, hivyo ni marukufu kwa mwanafunzi kutumia vifaa hivyo,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari Lindi yaliyoungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka huu.

Katika ajali hiyo, shule imeathirika kwa asilimia 34 na vyumba tisa vya madarasa, jengo lenye matundu 26 ya vyoo na jengo la maabara ya kemia na fizikia yameungua na kusababishia hasara ya Sh682.78 milioni.