Majaliwa aagiza kufunguliwa zahanati leo Bugabu

Muktasari:

Majaliwa amehoji sababu ya zahanati kutofunguliwa ilhali imekamilika na ina vifaa vyote vinavyotakiwa katika utoaji wa huduma.


Magu.Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza mganga mkuu wa Wilaya ya Magu, Dk Nindwa Maduhu ahakikishe zahanati Bugabu inafunguliwa leo Februari 18. 

Ametoa agizo hilo jana Jumamosi Februari 17, 2018  wakati akiongea na watumishi na wananchi wa Wilaya ya Magu katika Kituo cha Afya Kahangara.

Majaliwa amehoji sababu ya zahanati kutofunguliwa ilhali imekamilika na ina vifaa vyote vinavyotakiwa katika utoaji wa huduma.

Ametoa agizo hilo baada ya wananchi kumuomba awasaidie kufunguliwa kwa zahanati ya kijiji chao, ili kupata huduma za afya karibu. 

Wananchi hao wamedai kwamba wanalazimika kutembea umbali wa kilomita tisa kufuata huduma za afya katika Kituo cha Afya Kihangara.

Dk Maduhu amesema tayari watumishi walishahamishiwa katika zahanati ya kijiji hicho na leo wataanza kuwahudumia wananchi.

Kabla ya kuzungumza na wananchi na watumishi, Waziri Mkuu alikagua na kuweka jiwe la msingi la uboreshaji wa Kituo cha Afya Kahangara.

Mradi wa kuboresha kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia watu 26,321 ulianza Oktoba 30, 2017 na umegharimu Sh500 milioni.