Tuesday, July 17, 2018

Majaliwa aagiza viongozi wa ushirika kukamatwa

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Kahama. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza kamanda wa polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule kuwakamata viongozi wa Chama cha Msingi cha Mkombozi kwa upotevu wa Dola 21,000 za Marekani za chama hicho.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana alipozungumza na wananchi wa Kijiji cha Kangeme katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

“Wabebe hawa watu, wahoji waseme hiyo fedha iko wapi na jambo la kwanza wailete hiyo fedha ya wakulima, wakishindwa kurejesha wawekwe ndani,” alisema.

Agizo hilo alilitoa baada ya kuwaita viongozi wa chama hicho na kubaini hawakuwapo ikidaiwa walitoroka baada ya wananchi kuzomea.

Kamanda Haule aliwataja watuhumiwa kuwa ni mwenyekiti, Shilinde Abdallah; mhasibu wa chama hicho, Kulwa Shinzi na wajumbe saba wa bodi ya chama.

Katika mkutano huo, mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (Kacu), Emmanuel Cherehani alisoma taarifa akisema kuwa bei ya tumbaku ni nzuri, lakini wananchi walimzomea kupinga alichokisema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alisema kuna tatizo katika upangaji madaraja kwa kuwa wakulima wanalima tumbaku nzuri, lakini katika upangaji wa bei wakulima wanalipwa fedha kidogo.

Dk Tizeba alisema kuna wakulima wanakidai Chama cha Msingi cha Mkombozi madai ya tumbaku waliyouza tangu mwaka 2014.

-->