Majaliwa aeleza mbinu ya kuvutia wawekezaji nchini

Muktasari:

Awataka wakulima wa pamba kuongeza uzalishaji

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha lengo la Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda linafanikiwa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaboresha miundombinu ili kuvutia wawekezaji zaidi.

Akizungumza juzi na wafanyakazi alipotembelea Kiwanda cha Saruji cha Lake, kilichopo Kimbiji Wilaya ya Kigamboni, Majaliwa alisema Serikali itaboresha barabara zote zinazounganisha miradi mikubwa ya uwekezaji kwenye masoko.

 “Tunawapongeza wawekezaji wa kiwanda hiki kwa kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda. Tunawahakikishia Serikali itaboresha miundombinu ili bidhaa mnazozizalisha zifike sokoni wakati wote,” alisema.

Awali, akitoa taarifa ya utendaji kwa Waziri Mkuu, makamu wa rais mshiriki wa kiwanda hicho, Afroz Ansari, alisema walianza kuzalisha tani 296,000 za saruji mwaka 2014/15.

Alisema uzalishaji huo umeongezeka na kufikia tani 562,000 kwa mwaka 2016/17.

“Tuna uwezo wa kuzalisha mpaka tani milioni moja kwa mwaka, ila msimu wa mvua, kuna sehemu ya kilomita 36 zinazokiunganisha kiwanda hiki na barabara kuu eneo la Kibada haipitiki, hivyo tunalazimika kufunga kiwanda kwa muda, kwa kuwa tunashindwa kupeleka bidhaa zetu sokoni,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema kiwanda hicho kilichotoa ajira kwa watu 1,250, kimepoteza uzalishaji unaofikia tani 150,000 tangu kianze uzalishaji.

Baada ya kutoka kwenye kiwanda hicho kinachozalisha saruji ya Nyati, Majaliwa alitembelea kiwanda cha nyuzi cha Namera kilichoko Gongo la Mboto na kiwanda cha nguo cha Nida kilichopo Ubungo Dar es Salaam.

Majaliwa alisema safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia kutokana na uwapo wa viwanda vya kutengeneza nguo nchini.

Pia, alisema viwanda hivyo vitasaidia wakulima wa pamba kupata soko la uhakika, huku akiwataka kulima pamba ya kutosha ili viwanda vipate malighafi.

Alisema kutokana na viwanda hivyo, nchi iko njiani kuondokana na matumizi ya nguo za mitumba kwa kuwa nguo nyingi zitakuwa zinatengenezwa nchini na kupatikana kwa bei nafuu.

Majaliwa alisema kwa sasa wanunuzi wa pamba hawana sababu ya kwenda kuuza nje ya nchi, badala yake wauze katika viwanda vya ndani ili vizalishe nguo za kutosha. “Natoa wito kwa wakulima wetu wa pamba walime mazao ya kutosha kwa sababu soko la uhakika lipo na hii ndiyo safari ya mwisho ya mitumba.”