Majaliwa aeleza mafanikio ya Rais Magufuli

Muktasari:

  • Ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma, kutaja zaidi ya mambo 15 yaliyofanywa na Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani mwaka 2015

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais John Magufuli katika kipindi chake cha miaka mitatu ya uongozi, amefanikiwa kuimarisha nidhamu, uadilifu na uwajibikaji ndani ya utumishi wa umma na kukemea uzembe na kujenga ari ya kufanya kazi.

Mafanikio mengine ni ununuzi wa meli katika ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria; kufufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuimarisha usafiri wa anga na kukuza sekta mtambuka zikiwamo za utalii, afya, kilimo na kujenga reli ya kiwango cha kimataifa (SGR).

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 14, 2018 wakati akiahirisha mkutano wa 12 wa Bunge,  jijini odoma. Bunge limeahirishwa hadi Novemba 6, 2018.

Amesema mafanikio mengine yaliyofikiwa kipindi cha miaka mitatu ni kuendesha vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwenye taasisi za umma, sambamba na kuanzisha mahakama ya mafisadi na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi ikiwamo madini na maliasili.

“Kujenga vyanzo vipya vya umeme kama mradi wa kuzalisha umeme wa maji megawati 2,100 katika bonde la mto Rufiji (Stiegler’s Gorge); kusambaza umeme hadi vijijini na kuongeza kasi ya utekelezaji wa  miradi ya awamu ya tatu ya mpango wa Rea ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania),” amesema.

Waziri Mkuu amesema kiongozi mkuu huyo ameimarisha huduma za afya hususan upatikanaji wa dawa, vifaatiba katika vituo vya kutolea huduma za afya na ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za wilaya na utoaji elimu msingi bila malipo.

Amebainisha kuwa Rais amehakikisha miradi yote ya maji inayotekelezwa inakuwa bora, yenye uwiano na thamani halisi ya fedha na kukamilishwa kwa wakati na kuimarisha kilimo, ushirika na bei za mazao ya biashara.

Majaliwa amesema juhudi zote hizo zinafanywa kwa lengo la kuiwezesha nchi kufikia malengo ya dira ya Taifa ya kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo  2025.

“Niwaombe Watanzania wenzangu tuendelee kuunga mkono juhudi za Rais katika kuleta maendeleo,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa wawekezaji kutumia fursa ya uwapo wa mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, biashara na upatikanaji wa malighafi,  kwa kuja kujenga viwanda mbalimbali vikiwamo vya kuchakata mazao ya kilimo.