Majaliwa aitaka NEEC kutoka mikopo nafuu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa .

Muktasari:

  • Ametoa kauli hiyo leo wakati alipokutana na wajumbe wa baraza hilo katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi(NEEC), wakutane na wamiliki wa taasisi za kifedha ili kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo yenye gharama nafuu.

Ametoa kauli hiyo leo wakati alipokutana na wajumbe wa baraza hilo katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema ni vema wajumbe hao wakakutana na wamiliki wa taasisi hizo za kifedha ili kuwasaidia wananchi kupata mikopo yenye masharti nafuu itakayowawezesha kukuza uchumi wao.

“Baraza likutane na wamiliki hao na kuzungumza namna sahihi ya kuwezesha kutoa mikopo ya masharti nafuu. Pia tuangalie taasisi hizo  zinatuasadiaje sisi kama Serikali kuwawezesha Watanzania kupata mikopo ya masharti nafuu,” amesema.

Awali mwenyekiti wa baraza hilo, Dk John Jingu  alisema baraza  lilizinduliwa Januari 8, 2017 na walikubaliana kuanza kazi katika maeneo ya kipaumbele yatakayokuwa na tija kwa wananchi ambayo ni kilimo, sanaa, ufugaji na uvuvi.