Majaliwa aitaka TTCL ijitathmini

Muktasari:

Majaliwa alitoa agizo hilo katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana wakati akizindua mtandao wa 4G LTE wa kampuni hiyo.

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Kampuni ya Simu Tanzani kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya watumishi ili kupunguza gharama za uendeshaji.

Majaliwa alitoa agizo hilo katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana wakati akizindua mtandao wa 4G LTE wa kampuni hiyo.

Alisema matarajio ya Serikali ni kutaka kuona kampuni hiyo ikijiendeshe kwa faida badala ya kuomba ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Awali, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema Sh14.5 bilioni zilizolipwa kama fidia ya hisa kwa Kampuni ya Bharti Aitel zilitokana na biashara ya Mkongo wa Taifa. “Mkongo wa Taifa unafanya biashara vizuri, tunakuhakikishia kuwa tutausimamia vyema ili kuhakikisha unajenga na kuimarisha mawasiliano ya nchi nzima,” alisema.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kampuni hiyo, Waziri Kindamba alisema inazidai taasisi za umma Sh11.5 bilioni.

“Pamoja na mafanikio hayo, kampuni inakabiliwa na changamoto ya mtaji.

“Tunaomba utusaidie kuweka msisitizo kwa taasisi za umma tunazozidai Sh11.5 bilioni zilipe fedha hizi,” alisema Kindamba.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka kuthibitisha madeni husika kisha wakubaliane namna ya kuyalipa.

Kuhusu mitaji, Majaliwa aliitaka kampuni hiyo kufuata utaratibu unaohusika kushughulikia maombi yao ya fedha ili yafike kwenye mamlaka husika kwa hatua za uamuzi.