Majaliwa akaribisha ujenzi mpya Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Teknolojia hiyo inapotumika huwekwa jengo katika umbile lolote analotaka mhusika, huku kemikali inayotumika ikiwa ni salama kiafya na huhifadhiwa kama kimiminika katika mapipa.

Pwani. Unataka kujenga? Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kimegundua teknolojia inayotumia mchanganyiko wa kawaida wa saruji, mchanga na maji vinavyochanganywa kwa uwiano maalumu pamoja na dawa iitwayo Moladi Chem.

Teknolojia hiyo inapotumika huwekwa jengo katika umbile lolote analotaka mhusika, huku kemikali inayotumika ikiwa ni salama kiafya na huhifadhiwa kama kimiminika katika mapipa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza teknolojia hiyo ya ujenzi wa nyumba nafuu inayofahamika pia kwa jina la Moladi itumike kwenye majengo ya Mahakama na makao makuu mjini Dodoma.

Majaliwa alisema hayo jana mjini Kibaha baada ya kushuhudia jengo la Mahakama lililojengwa na Chuo Kikuu Ardhi (Aru) kwa teknolojia hiyo, lililogharimu Sh520 milioni badala ya Sh1.3 bilioni zilizokuwa zitumike kwa mfumo wa awali.

Jaji Mkuu Mohamed Chande, alisema mpango mkakati wa miaka mitano kwa Mahakama ni uboreshaji, utawala bora, uwajibikaji, usimamizi wa rasilimali, upatikanaji wa haki kwa wakati na uimarishaji wa imani kwa wananchi.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrissa Mshoro alisema Juni 2014 baada ya kupewa jukumu la kufanya utafiti wa teknolojia mwafaka ya ujenzi, waligungua Moladi itawezesha Mahakama kupata majengo bora, yenye gharama nafuu na kwa muda mfupi, huku ikiwa ni rafiki wa mazingira.