Majaliwa amaliza mgogoro uliodumu miaka minne

Muktasari:

  • Ufumbuzi wa mgogoro umetokana na Serikali kutengua uamuzi wa kujenga makao makuu hayo eneo la Nyamwaga, baada ya kubaini kuwa haukufuata taratibu ikiwamo mahitaji ya kijiografia ya kusogeza huduma karibu na wananchi.

Tarime. Hatimaye Serikali imetatua mgogoro uliodumu kwa miaka minne wa eneo linalotakiwa kujengwa makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Tarime.

Ufumbuzi wa mgogoro umetokana na Serikali kutengua uamuzi wa kujenga makao makuu hayo eneo la Nyamwaga, baada ya kubaini kuwa haukufuata taratibu ikiwamo mahitaji ya kijiografia ya kusogeza huduma karibu na wananchi.

Akitangaza uamuzi huo juzi Januari 17 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitaja sababu nyingine kuwa ni hasara ambayo halmashauri itapata kwa kulazimika kuwalipa fidia wananchi watakaohamishwa kupisha makao makuu hayo.

Katika mkutano wake na madiwani na watumishi wa halmashauri ya wilaya na mji wa Tarime, Majaliwa alisema Serikali itatuma upya wataalamu kufanya utafiti kwa kutembelea eneo lote la halmashauri hiyo na kutoa ushauri wa sehemu inayofaa kuwa makao makuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliiagiza ofisi ya mkuu wa wilaya ya Tarime kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua maofisa na wataalamu wa ardhi wanaotuhumiwa kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi wilayani hapa.

“Haiwezekana wataalamu wa ardhi washindwe kutatua migogoro inayohusiana na mipaka wakati wanayo ramani inayoonyesha mipaka yote, hawa ndiyo chanzo cha matatizo kwa kugawa kiwanja kimoja kwa watu wawili kutokana na kuendekeza rushwa. Washughulikiwe!” aliagiza Mjaliwa.