Majaliwa ampa jukumu CDF Mabeyo

Muktasari:

  • Majaliwa ametaka hadi kufikia leo Septemba 24, 2018 saa 10:00 jioni awe amepata mwelekeo wa shughuli ya uokoaji na unyanyuaji wa kivuko cha MV Nyerere

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kazi ya uvutaji kivuko cha Mv Nyerere kilichozama na uokoaji wa miili zitafanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) chini ya Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo.

Akizungumza leo Septemba 24, 2018 eneo la kisiwa cha Ukara ambako shughuli za mazishi ya watu waliozama kwenye kivuko cha MV Nyerere inaendelea, Waziri Mkuu amesema jukumu hilo litakuwa chini ya Mkuu wa Majeshi.

Amesema kazi hiyo ipo mikononi mwake na anaamini majeshi hayana vikao vingi akihitaji msaada wowote amwambie waziri mwenye dhamana au mkuu wa mkoa.

Majaliwa amesema shughuli ya uibuaji kivuko hicho isichukue muda mrefu, “Ile kauli ya awali ya shughuli hiyo kuchukua wiki moja haipo, nataka hatua hii imalizike haraka iwezekanavyo.”

“Kazi hii inatarajiwa kuongeza idadi ya watu walioko huko chini ya kivuko, hivyo utaratibu wa namna ya kuzitambua ufanyike”

Majaliwa amesema anataka kufikia saa 10:00 jioni ya leo apate taarifa kamili ikiwamo mwelekeo wa hatua ya uibuaji meli hiyo.

Amesema miili yote itakayotolewa chini ya kivuko hicho itakuwa imeharibika sana, hivyo kama kutakuwa na miili inayoweza kutambulika kwa ajili ya nguo lifanyike hilo kwa muda kidogo kabla ya kuipeleka kwenye makazi yao ya milele.

Majaliwa amesema mbali na hilo miili hiyo ipimwe vina saba (DNA) ili kusaidia iwapo kuna ndugu watasema hawajawaona jamaa zao waweze kuitambua.

Ameagiza kazi hiyo iendelee kwa kasi ya hali ya juu.

“Nimekuja kutoa maelekezo hayo kuwa CDF (Mabeyo) chukua nafasi ya shughuli hii  na kama kuna vifaa unahitaji mkuu wa mkoa ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama yupo utaomba kila kitu unachohitaji, ”amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema kama kuna vyombo vingine vya kusaidia kunyanyua hicho kivuko kipo Mwanza kinatakiwa kiwe kimeshafika hapo.