Majaliwa amtwisha zigo RC wa Katavi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Alitoa agizo hilo alipokuwa akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kiwanja cha Inyonga, wilayani Mlele.

Katavi. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga kupeleka wakaguzi wilayani Mlele kubaini watu waliokula fedha za Chama cha Ushirika Ukonongo na kuwachukulia hatua.

Alitoa agizo hilo alipokuwa akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kiwanja cha Inyonga, wilayani Mlele.

Majaliwa alisema kila mtumishi afanye kazi na awajibike kwa uadilifu na uaminifu kwa mujibu wa taaluma yake, ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kwani hilo ndilo lengo la kuajiriwa kwao.

“Haiwezekani hapa kuna ofisa ushirika halafu Waziri Mkuu analetewa mabango ya kumtaka atatue tatizo la chama cha ushirika. Hali hii inaonyesha hakuna kazi inayofanyika,” alisema.

Majaliwa alisema wanahitaji watumishi watakaosikiliza maelekezo yanayotolewa na Serikali na kuyafanyia kazi.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kupandishwa hadhi kwa Kituo cha Afya Inyonga kuwa hospitali ya wilaya.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kassanda alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa nyumba za watumishi, hali inayosababisha yeye (Kassanda) na katibu tawala wake kuishi nyumba za kupanga.