Majaliwa asema hakuna kugawa maeneo mapya ya utawala

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa 

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa  kwa vyombo vya habari leo  Jumamosi Agosti 12 na Ofisi ya Waziri ilieleza kuwa Majaliwa alitoa kauli katika mkutano wa hadhara wa eneo  Ulyankulu na Kaliua mkoani Tabora akiwa kwenye ziara yake ya kikazi.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imesitisha mchakato  kutoa maeneo mapya ya utawala hadi itakapotangazwa vinginevyo.

Taarifa iliyotolewa  kwa vyombo vya habari leo  Jumamosi Agosti 12 na Ofisi ya Waziri ilieleza kuwa Majaliwa alitoa kauli katika mkutano wa hadhara wa eneo  Ulyankulu na Kaliua mkoani Tabora akiwa kwenye ziara yake ya kikazi.

"Tumesitisha mchakato wa kutoa maeneo mapya ya utawala ili tuimarishe kwanza yale ya awali. Tunaimarisha kwanza miundombinu ya majengo ya ofisi, nyumba za watumishi kwenye wilaya na halmashauri mpya na zikitengamaa tutafanya uamuzi upya," alisema Majaliwa katika taarifa hiyo.

 Majaliwa ambaye pia ni Mbunge Ruangwa (Lindi) alieleza hayo wakati akijibu  maombi ya wabunge wa majimbo ya Ulyankulu na Kaliua  walisema kuna haja ya kuigawa wilaya ya Kaliua ili kusogeza huduma kwa wananchi waishio kwenye kata zilizo mbali na tarafa.