Majaliwa asema michango ya Watanzania, itatumika kujenga mnara, uzio

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema baadhi ya michango inayochangwa kwa ajili ya waathirika wa ajali ya Kivuko cha MV Nyerere itatumika kujenga uzio na mnara katika eneo walilozikwa la Ukara

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema baadhi ya pesa zitakazopatikana katika michango ya Watanzania zitatumika kujenga uzio na mnara katika makaburi ya watu waliokufa katika ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.

Fedha hizo zinachangwa kupitia akaunti maalumu iliyofunguliwa katika benki ya NMB pamoja na namba maalumu ya Tigo kupitia simu ya mkononi.

Akizungumza katika shughuli ya mazishi leo Septemba 23,2018 visiwani Ukawa wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza amesema baadhi ya miili ya watu waliokufa katika ajali hiyo fedha hizo hazitatumika katika shughuli yoyote nje ya tukio hilo.

"Fedha hizi ni za wafiwa hivyo hatuna budi kuzitumia kulingana na mwenendo wa tukio," amesema Majaliwa.

Amesema ili kuhakikisha wananchi wa eneo hilo hawapati tabu Serikali iko katika mkakati wa kuleta kivuko cha muda.

"Tutafanya ukarabati wa kutosha katika baadhi ya vivuko ikiwemo Mv Misungwi, Sengerema ili kuimarisha usafiri wa majini katika maeneo yote," amesema Kassim.

Majaliwa amewaomba Watanzania kuwatia moyo wafiwa badala ya kuwaambia maneno yanayoweza kuwasababishia maumivu.

"Watu hawa wamepoteza ndugu zao wa muhimu hivyo ni vyema kuwapatia maneno mazuri yanayotia moyo badala ya kuwajaza maneno ya upotoshaji na tuiache Serikali ifanye jitihada zake," amesema Majaliwa.

Amesema muda wowote kuanzia sasa tume ya uchunguzi itaundwa ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na Serikali ikiwa tayari iko katika mazungumzo juu ya matumizi ya Meli ya Mv Nyahunge.

Kivuko cha Mv Nyerere mpaka sasa takwimu zinaonyesha kilikuwa na watu 265 ambao kati yake 224 wamepatikana wakiwa tayari wamepoteza maisha huku 41 wakipatikana wazima.