Majaliwa atoa tamko usimamizi wa madini

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani(katikati) wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Mtaalamu wa Jiolojia, Timo Gawronski,walipotembelea maabara zilizopo kwenye kituo cha madini(AMGC).

Muktasari:

  • Mkutano umehitimishwa kwa kusherehekea miaka 40 tangu kuanzishwa Kituo cha Madini Afrika mwaka 1977.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuandaa mikakati madhubuti ya kusimamia sekta hiyo kwa manufaa ya Taifa.

Amesema hayo alipofunga mkutano wa 37 wa ngazi ya mawaziri wa nishati na madini wa nchi wanachama wa Kituo cha Madini Afrika (AMGC) uliolenga kujadili mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya bara hilo.

Mkutano huo umefanyika leo Alhamisi katika kituo cha AMGC kilichopo jijini hapa, Tanzania ikiwa mwenyekiti.

Waziri mkuu amesema licha ya nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania kuwa na utajiri wa madini, sekta hiyo haina tija kwa maendeleo hivyo ameagiza kuandaliwa mikakati madhubuti.

"Bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa madini, sehemu kubwa ya madini hayo hayajatumika. Tanzania ina madini mengi kama vile dhahabu, almasi na Tanzanite lakini mchango wake ni asilimia nne pekee," amesema.

Kutokana na hali hiyo, amezitaka nchi wanachama wa AMGC kuandaa mikakati ya pamoja ili madini yawanufaishe wananchi.

"Changamoto iliyopo ni jinsi gani tunaweza kusimamia sekta hizi na kuleta maendeleo kuliko kuacha mashimo na umasikini," amesema.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani amesema wamepokea maagizo hayo na kuanzia mwakani watatumia kituo hicho kuchenjua mchanga wa madini na kufanya uyeyushaji.

"Nitoe wito kwa kampuni za madini na wachimbaji wadogo kuanza kuleta madini kwenye kituo hiki kwa ajili ya kuongeza thamani na kufanya uchambuzi," amesema