Majaliwa awasili Ukara, kushuhudia kivuko kikinyanyuliwa

Muktasari:

  • Shughuli ya kukinyanyua kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka Septemba 20, 2018 imeanza chini ya usimamizi wa wataalam wa masuala ya majini kutoka vyombo vya ulinzi na usalama wakishirikiana na wenzao kutoka kampuni ya Songoro Marines ya jijini Mwanza

Ukara. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasili kijiji cha Bwisya kisiwa cha Ukara kuongoza na kushuhudia kazi ya kukinyanyua kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka Septemba 20.

Helkopta iliyomleta kiongozi huyo imetua kijiji cha Bwisya saa 4:00 asubuhi leo Septemba 24,2018.

Hadi leo asubuhi, mwili mmoja umepatikana hivyo kufikisha idadi ya watu 225 waliofariki katika ajali hiyo.

Tayari kazi ya kupanga zana na vifaa vya kunyanyua kivuko hicho inaendelea chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Mv Nyerere, Isaac Kamwelwe ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Viongozi wengine wanaoshuhudia shughuli hiyo tangu saa 3:30 asubuhi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Kazi na Walemavu) Jenister Mhagama, Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeho.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema kazi hiyo inafanyika kitaalam kuhakikisha kivuko hicho kinanyanyuliwa na baadaye kugeuzwa.