Majaliwa awataka NHC kuelekea makazi mapya

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Muktasari:

Kwa upande wake, mbunge wa jimbo la Momba, David Silinde aliishukuru Serikali kwa kujenga nyumba hizo na kusisitiza kwamba maendeleo hayana chama.

Songwe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Nyumba Nchini (NHC) kwenda kujenga nyumba bora za makazi katika maeneo yote mapya ya utawala ikiwemo mikoa na wilaya ili kusaidia kutatua changamoto ya makazi kwa watumishi.

Waziri Mkuu pia ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Momba mkoani Songwe zinazojengwa na NHC katika kijiji cha Tindingoma.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Naming’ongo wilaya ya Momba akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Songwe.

“Nalipongeza Shirika la Nyumba kwa mikakati waliyonayo, waendelee na utekelezaji wa mipango ya ujenzi wa nyumba ili maeneo yote mapya ya utawala yaweze kuwa na makazi bora ya kuishi watumishi.”

Pia aliwataka wakazi wa kata ya Chitete yaliko makao makuu ya wilaya ya Momba kuhakikisha wanachangamkia fursa ya uwepo wa makao makuu wa wilaya kwenye kata yao kwa kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya kupangisha watumishi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu amesema mradi huo wenye thamani ya Sh 2.2 bilioni, ulianza kujengwa Machi 2016 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.

Amesema mradi huo ulibuniwa baada kupokea maombi kutoka halmashauri ya wilaya ya Momba na kwamba unatekelezwa kwa awamu mbili, ya kwanza ni ujenzi nyumba nane na tayari zimekamilika.

Ameongeza kwamba ujenzi wa awamu ya pili unajumuisha nyumba tisa ambapo gharama ya ujenzi wa nyumba itatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya ofisi za halmashauri hiyo.

Pia mbunge wa jimbo la Momba, David Silinde amesema anaishukuru Serikali kwa ujenzi wa nyumba hizo na kumueleza Waziri Mkuu kwamba wananchi wa Momba wanaridhishwa na utendaji wa Serikali na kwamba maendeleo hayana chama.