Majaliwa awatwisha mzigo ma-RC

Muktasari:

  • Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maghala na vihenge vya kisasa kwa kanda nane uliogharimu Dola55 milioni za Marekani (zaidi ya Sh115 bilioni) uzinduzi uliofanyika mjini Dodoma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya na mikoa ambayo inalima mazao ya kimkakati kusimamia vyama vya ushirika vilivyopo kwenye maeneo yao kwa kuwa ndio mkombozi wa wakulima.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maghala na vihenge vya kisasa kwa kanda nane uliogharimu Dola55 milioni za Marekani (zaidi ya Sh115 bilioni) uzinduzi uliofanyika mjini Dodoma.

Alisema kuwa hapo awali vyama vingi vya ushirika vilikuwa vinakimbiwa kwa kuwa kulikuwa na upungufu wa aina mbalimbali ambao tayari Serikali imeshaufanyia marekebisho.

Majaliwa alisema dhamira ya kujenga vyama vya ushirika ni ya dhati kwa sababu vilivyokuwepo awali vilipoteza matumaini ya ushirika kwa wakulima na kuwepo kwa makundi ya watu wasiokuwa waadilifu waliokuwa wanatumia ushirika vibaya.

“Ushirika sasa ni lazima tuusimamie kwa nguvu na wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kama wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yenu hakikisheni vyama vya msingi vya ushirika na vyama vikuu vya ushirika vinakuwa na viongozi waadilifu waaminifu na wale ambao wanajali kazi nzito waliyoifanya wakulima wenzao,” alisema.

Pia, alisema moja ya masharti ya kiongozi wa ushirika ni lazima awe mkulima ili aweze kuona uchungu wa uhifadhi na kuongoza vizuri kwenye eneo hilo.

Aliongeza kuwa, wameimarisha mkakati huo kutoka Wizara ya Kilimo kwa kuwa ushirika ndio njia sahihi inayomwezesha mkulima kupata pembejeo, viuatilifu na mahitaji ya kitaalamu ni rahisi kumfikia kupitia ushirika.

Alisema mazao yote ya mkakati ni lazima yaundiwe vyama vya ushirika kama vile kahawa, pamba, tumbaku na chai.

Waziri mkuu alipiga marufuku kwa mtu yeyote kwenda kwa mkulima mmoja mmoja kununua mazao kwa bei ndogo, bali mazao yote yapitie kwenye vyama vya ushirika ili wanunuzi waweze kupambanishwa kwenye minada.

Waziri wa Kilimo na Chakula, Dk Charles Tizeba alisema kuwa japokuwa msimu huu mvua imenyesha kubwa, lakini kumekuwapo na wadudu waharibifu ambao wamevamia mazao ya wakulima na kusababisha hasara kubwa wakiwemo viwavijeshi waliotoka barani Amerika. Dk Tizeba alisema kuna idadi kubwa ya panya wanaoharibu mazao katika mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro na Dodoma na kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote ambao maeneo yao yamevamiwa na panya hao kutoa taarifa wizarani ili watume sumu ya kuwaangamiza.s