Majaliwa azungumzia magonjwa yasiyoambukiza

Muktasari:

Majaliwa ameyazungumza hayo leo wakati akifungua mkutano wa 65 wa mawaziri wa afya wa Jumuiya za nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa bara la Afrika uliowashirikisha mawaziri kutoka nchi tisa.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mapambano ya magonjwa yasiyoambukiza yatafanikiwa endapo sekta nyingine mbali na afya zitashirikishwa.

 

Majaliwa ameyazungumza hayo leo wakati akifungua mkutano wa 65 wa mawaziri wa afya wa Jumuiya za nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa bara la Afrika uliowashirikisha mawaziri kutoka nchi tisa.

 

Amesema kutokana na ongezeko la magonjwa hayo, nchi hizo zinapaswa kuangalia namna ambavyo zitatatua ongezeko hilo ili kupunguza gharama.

 

"Ili kuepuka  kutumia gharama kubwa katika kutibu magonjwa haya juhudi za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ikiwemo kushirikisha sekta nyingine katika kutatua changamoto zilizopo lakini zaidi ni kuelimisha jamii kubadili mfumo wa maisha," amesema Majaliwa.

 

Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia (WB), Dk Paolo Belli amesema nchi hizo kwa sasa zinatakiwa kutumia teknolojia mpya ili kupata matokeo mapya katika magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa yasiyoambukiza, TB na vifo vya wajawazito na watoto.

 

Aidha, amezishauri nchi hizo kuangalia uwezekano wa kupunguza matumizi ya tumbaku kwa kuwa  yanasababisha madhara kwa watu wengi ikiwemo gharama za kutibu magonjwa mengi yatokanayo na madhara ya tumbaku.