Majaliwa kufungua maonyesho ya utalii Dar

Muktasari:

Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa anatarajiwa kufungua maonyesho ya nne ya kimataifa ya utalii wa Swahili (SITE) yatakayofanyika Oktoba 12 hadi 14 yakishirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi


Dar es salaam. Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa anatarajiwa kufungua maonyesho ya kimataifa ya utalii ya Swahili (SITE) yatakayoanza Oktoba 12 hadi 14 Dar es Salaam.

Akizungumza leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii, Devota Mdachi alisema lengo kuu la maonyesho hayo ni kuwaunganisha wafanyabiashara wadogo na wakati wa utalii Tanzania na kutoka masoko makuu ya utalii duniani.

Alisema maonyesho hayo yananyika kwa mara ya nne nchini lakini yatakuwa tofauti kutokana na kuwaalika mawakala wengi zaidi tofauti na miaka mingine.

“Maonyesho haya yanatarajiwa kuhudhuriwa na kampuni 170 kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika na ukanda wa bahari ya hindi pamoja na wafanyabiashara wa kimataifa na vyombo vya habari 300,” alisema Mdachi.

Alisema mawakala hao watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii katika kanda ya Kusini pamoja na maeneo ya Pangani Tanga na Mafia.

Meneja Masoko na Mauzo kutoka kampuni ya uongozaji utalii hapa nchini (Ocean Cruising Safaris) LTD) ambaye ni mdhamini mkuu, Christine Jengo alisema maonyesho hayo ni tofauti kwa kuwa wameanzisha boti maalum kwa ajili ya utalii.

“Ili kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa nchini tumeona ni muhimu kuifanya tofauti kwa kuanzisha boti maalum zitakazokuza utalii wa ndani,” alisema Jengo.

Alisema katika maonyesho hayo mawakala hao pia watapata fursa ya kujionea mambo  mbalimbali ikiwamo nyuki pamoja na mvinyo.