Majaliwa kufungua maonyesho ya wiki ya Azaki

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kesho atafungua wiki ya Azaki ya mwaka 2018 yanayoanza jijini hapa na kumalizika Oktoba 30, 2018  ambapo asasi zaidi ya 250 nchini zitashiriki

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kesho atafungua maonyesho ya wiki ya Asasi za Kiraia (Azaki) mjini hapa yatakayoshirikisha washiriki zaidi ya 800 kutoka asasi zaidi ya 250.

Washiriki wengine wa maonyesho hayo ni kutoka serikalini pamoja na bungeni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation of Civil Society, Francis Kiwanga amesema leo Oktoba 21, 2018 kuwa wiki hiyo itaanza kesho na kumalizika Oktoba 26, 2018  jijini hapa.

Kiwanga amesema washiriki hao watashiriki katika maonyesho na midahalo kujadili ajenda  ya kujenga Tanzania ya Uchumi wa Viwanda kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya miaka mitano.

Amesema wiki hiyo inalenga katika kutoa nafasi kwa sekta ya asasi za kiraia (Azaki) kuwapa wananchi nafasi na ushiriki kwenye juhudi za Serikali na wadau wengine za kujenga uchumi wa viwanda.

“Azaki pia zinalenga katika kuhamasisha ujenzi wa jamii inayoheshimu haki za watu na kuwashirikisha raia wake katika michakato ya mustakabali wa maisha yao,” amesema.

Amesema wiki hiyo itatoa fursa ya majadiliano na mabadilishano ya taarifa na uzoefu kuhusu ushiriki mpana wa wananchi katika ujenzi wa utaifa wao.

Amesema pia wiki hiyo itaunganisha washiriki kupitia fursa mbalimbali za mashirikiano na Serikali na taasisi zake, Bunge na wadau wengine.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Wajibu, Ludovick Utouh amesema jukumu kubwa la Azaki ni kuelimisha na kuhamasisha uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za msingi na pia kuwezesha ushiriki wao katika michakato ya maendeleo ya Taifa.

“Azaki inatoa fursa na jukwaa la kushiriki katika michakato yote ya maendeleo ya jamii ikiwemo elimu, afya, kilimo na ufuatiliaji wa uwajibikaji kwa jamii na matumizi ya raslimali za umma,” amesema.