Majaliwa kuhamia Dodoma leo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Muktasari:

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma imeandaa mapokezi ya Waziri Mkuu atakapowasili mchana na kuanzia kesho atafanya ziara ya siku mbili katika manispaa ya Dodoma kukagua hatua za maandalizi ya kupokea ujio wa Serikali.

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuhamia rasmi leo mjini hapa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Julai 25, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma imeandaa mapokezi ya Waziri Mkuu atakapowasili mchana na kuanzia kesho atafanya ziara ya siku mbili katika manispaa ya Dodoma kukagua hatua za maandalizi ya kupokea ujio wa Serikali.

Taarifa ya ofisi ya mkoa imesema Majaliwa atatembelea maeneo ya kutolea huduma za afya, kituo cha umeme cha Zuzu, masoko, chanzo cha maji cha Mzakwe na maeneo ya viwanda.

Ofisa habari wa mkoa, Jeremiah Mwakyoma amesema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mapokezi hayo yamekamilika.