Majambazi waua mfanyabiashara mita 20 karibu na kituo cha polisi

Mfanyabiashara Godfrey Ndosi (40) aliyeuawa.Picha na Daniel Mjema

Muktasari:

  • Watu walioshuhudia tukio hilo lililotokea saa 2:00 usiku, walidai baada ya kusikika kwa milio hiyo ya risasi, polisi waliokuwa katika kituo hicho walizima taa kwa tahadhari na wengine kutoka nje.

Moshi. Watu wawili waliokuwa na bunduki aina ya SMG, juzi usiku walitikisa eneo la Kiborlon mjini Moshi kwa kufyatua risasi kadhaa, hatua 20 kutoka kituo kidogo cha polisi Kiborlon na kumuua mfanyabiashara Godfrey Ndosi (40)

Watu walioshuhudia tukio hilo lililotokea saa 2:00 usiku, walidai baada ya kusikika kwa milio hiyo ya risasi, polisi waliokuwa katika kituo hicho walizima taa kwa tahadhari na wengine kutoka nje.

Ingawa gari la doria la polisi ambalo halikuwa mbali na eneo hilo, lilifika kwa wakati lakini majambazi hao walifanikiwa kutoroka wakitembea kwa miguu, kupitia uchochoro uliopo nyuma ya kituo hicho.

Tukio la kuuawa kwa mfanyabiashara huyo  maarufu kwa jina la G bila watu hao kuiba chochote, limeibua hisia tofauti hasa kutokana na ukweli amekoswakoswa mara mbili na kundi hilo.

Hata hivyo, baada ya watu hao kushindwa kupora dukani kwa marehemu, mmoja aliingia katika duka la muuzaji wa jumla wa bia na kufanikiwa kuiba kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakijajulikana.

Diwani wa Kata ya Kiborlon (Chadema), Frank Kagoma ambaye alifika eneo la tukio muda mfupi baadaye, alidai watu hao walifanikiwa kutoroka kutokana na taharuki iliyolikumba eneo hilo.

“Nilivyoelezwa ni kuwa walikuja watu wawili mmoja amevaa koti akamkuta marehemu anaongea na marafiki zake. Huyo mmoja akawa kama amemsukuma aingie dukani kwake,”amesema Kagoma.

Kwa mujibu wa kagoma, mtu huyo alifunua koti na kutoa bunduki ya kivita na kumfyatulia risasi zisizopungua sita kifuani, ambapo alianguka kifudi fudi na majambazi wakavamia duka jirani.

“Wakati huyo mwenye silaha anaingia kwenye duka la bia akapishana na mama ambaye ndio mmiliki akitoka akikimbia kwa hofu. Jamaa aliingia akavuta droo akachukua pesa na vocha za simu,”amesema.

Diwani huyo alidai ana mashaka bunduki hiyo ndio imekuwa ikilisumbua eneo hilo na maeneo ya jirani, akidai ana mashaka wanaotenda matukio hayo waliachilia hivi karibuni toka gerezani.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Hamisi Issah alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akiwataka wananchi na wakazi wa mkoa huu kutoa taarifa na kuwafichua watu waliotekeleza mauaji hayo na uporaji.