Drones zaanza majaribio ya kusambaza dawa

DRONE KUTUMIKA KWA MAJARIBIO KUSAMBAZA DAWA NCHINI

Muktasari:

Teknolojia na usafirishaji utagharimu zaidi ya Sh1.5 bilioni.

Mwanza. Tatizo la upungufu wa dawa na vifaa tiba kwa zaidi ya wakazi 300,000 wanaoishi katika visiwa zaidi ya 30 vilivyoko ndani ya Ziwa Victoria mkoani Mwanza umepata ufumbuzi baada ya kikwazo cha usafiri kutatuliwa.

Hii ni baada ya mkoa huo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia (WB), kuzindua mradi wa majaribio wa kutumia ndege maalumu zisizo na rubani (drones) kusambaza dawa na vifaa tiba katika visiwa hivyo.

Mradi huo wa majaribio utakaohusisha pia mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya afya, teknolojia na usafirishaji utakaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh1.5 bilioni umezinduliwa leo Jumanne Desemba 12,2017 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.

Wadau wengine watakaochangia gharama za mradi huo ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), Serikali na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Mtaalamu wa teknolojia kutoka WB, Edward Charles amesema mradi huo pia utahusisha masuala ya utafiti, ubunifu na usalama.

Akizungumzia matumizi ya teknolojia hiyo, Mongella amesema mradi huo si tu utarahisisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, bali pia utaokoa maisha ya wakazi wa visiwa hivyo waliokuwa wakikosa huduma za haraka wakati wa dharura.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu amesema teknolojia inaweza kupunguza gharama ya zaidi ya Sh3 bilioni zinazotumika sasa kusambaza dawa na vifaa tiba katika vituo zaidi ya 7,000 nchini.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Leonard Subi amesema teknolojia hiyo itasaidia utoaji wa huduma ya chanjo kwa  wajawazito na watoto;  ukusanyaji na usambazaji wa damu katika zahanati na vituo vya afya vilivyoko katika visiwa hivyo.

Mhandisi, George Mulamula kutoka Costech amesema mafanikio ya mradi huo wa majaribio katika mikoa ya Kanda ya Ziwa yatasaidia teknolojia hiyo kusambazwa na kutumika katika mikoa mingine nchini na hasa ya pembezoni yenye changamoto ya usafishaji.