Majigambo ya uchaguzi yaendelea

Mgombea ubunge Jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya CCM, Maulid Mtulia akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika jana katika Uwanja wa Vegas, Kijitonyama jijini Dar es Salaam. Picha na Venance Nestory

Muktasari:

  • Wakihutubia mikutano ya hadhara jana, wagombea wa CCM, CUF na Chadema wamewaomba wananchi kuitumia Februari 17 kuwachagua, huku wakipigana vijembe.

Dar/Moshi. Zikiwa zimebaki siku tisa kufanyika uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni na Siha, wagombea katika majimbo hayo wameendeleza majigambo wakiomba kuchaguliwa.

Wakihutubia mikutano ya hadhara jana, wagombea wa CCM, CUF na Chadema wamewaomba wananchi kuitumia Februari 17 kuwachagua, huku wakipigana vijembe.

Akiwahutubia wakazi wa Magomeni Idrisa, mgombea wa CUF Kinondoni, Rajabu Salum alisema wazee wa CCM wamemweleza anawafaa kuwa mbunge wao na wameshtushwa na uamuzi wa chama chao kumpa dhamana Maulid Mtulia.

“Wazee hao wamekasirika na wameamua kurejesha kadi zao za chama (huku akionyesha kadi 10 za CCM). Niwaeleze kuwa katika uchaguzi huu hakuna Ukawa wala upawa na ninasikitishwa na wana CUF kuwaunga mkono Chadema,” alisema Rajabu.

Aliahidi akichaguliwa atatenga fedha kwa ajili ya walimu watakaofaulisha wanafunzi na kuishauri Serikali kutenga fedha ili watoto wapate walau mlo mmoja wakiwa shuleni.

Awali akimnadi Rajabu, mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya alisema ikifika siku ya kupiga kura Februari 17 wasihukumiane kwa makosa aliyofanya Mtulia ambaye ni mgombea wa CCM jimboni Kinondoni.

Mtulia alikuwa mbunge jimboni humo kupitia CUF, lakini alijiuzulu na kujiunga na CCM.

Mrudisheni Mtulia

Mgombea huyo wa CCM katika mkutano uliofanyika Kata ya Makumbusho Uwanja wa Vegas aliwaomba wananchi wa Kinondoni wamchague tena.

“Mimi nina asili ya Makumbusho zamani ilikuwa Mwananyamala. Mimi nina bahati ya kuwa na familia, mtoto wangu alifariki. Chagueni mtu anayejua shida zetu msichague mtu asiyejua shida zenu,” alisema Mtulia.

Alisema, “Mimi nimesoma Shule ya Msingi Tandale, nimebeba mchanga ili ninunue kiatu. Mimi nimepambana sana, lakini unapokuwa mbunge wa upinzani utafanya nini? Nilipokuwa mbunge wa upinzani nilisimamia ila sikuweza.”

Awali, mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde maarufu kibajaji akihutubia mkutano huo alisema, “Leo (jana) niko hapa Serikali yote inajua. Nikitoka hapa simu ya kwanza ni ya mukulu, ataniuliza tutashinda namwambia tutashinda, ila Mtulia ana shida ya maji.”

Dk Godwin Mollel wa CCM anayegombea ubunge Siha akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Ormelili cha jamii ya wafugaji alisema elimu ndiyo urithi pekee ambao wazazi wanaweza kuwarithisha watoto, hivyo ni vyema wakazingatia hilo ili kujihakikishia maendeleo.

Dk Mollel, ambaye hivi karibuni aliihama Chadema na kurudi tena kuomba kura kupitia CCM alisema akishinda atahakikisha anaboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili watoto waweze kupata elimu bora na kujiletea maendeleo.

Alisema lengo la kuomba nafasi hiyo si ili kupata heshima, bali kuwaletea wananchi maendeleo na kuwaondoa kwenye changamoto zinazowatesa zikiwemo za miundombinu mibovu ya barabara, ukosefu wa umeme, huduma bora za afya na maji.

Mgombea wa Chadema Jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu akihutubia mkutano wa hadhara Tandale kwa Tumbo alisema, “Fursa ninayoitafuta ni kuwaunganisha wananchi wa Kinondoni bila kujali tofauti zao za kidini, kiitikadi wala kiuchumi. Kuna watu wanazunguka huko na kusema Salum Mwalimu ni Mzanzibari, aliyewaambia mimi ni Mtanganyika nani?”

Mwalimu alisema, “Kwani kuwa Mzanzibari ni dhambi? Tunachotafuta ni mtu wa kwenda kuwatetea wananchi, Tanzania yetu ni moja.”

Alisema Benki ya Dunia imetoa fedha kwa ajili ya kujenga Mto Ng’ombe ili mvua zinaponyesha zisibebe takataka na kuchafua mazingira.

“Fedha za kulipa fidia zimetolewa kwa wale watakaoguswa na mradi huo. Ninawaahidi kwamba hakuna mtu atakayehamishwa bila kulipwa fidia kuanzia Tandale mpaka kule mwisho,” alisema Mwalimu.

“Unapochagua mbunge asiye na uwezo wa kujenga hoja, unapochagua mbunge ambaye hawezi kumwambia Rais Magufuli hapana, suala la maendeleo hakuna,” alisema.

Awali, katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo alisema hakuna kura hata moja ya mwananchi itaibwa kwa sababu wamejipanga.

Imeandikwa na Elias Msuya, Peter Elias, Kalunde Jamal, Fortune Francis na Elizabeth Edward (Dar) na Florah Temba (Moshi).