Uhamiaji yaanika watumishi walioacha kazi

Muktasari:

Uamuzi wa Uhamiaji kuweka hadharani majina hayo ni kuisaidia jamii kuwatambua.


Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji imewatahadharisha wananchi kuwa makini na waliokuwa watumishi wake walioacha kazi kwa sababu mbalimbali ikiwamo kufukuzwa kati ya mwaka 2016/17.

Akizungumza na gazeti hili leo Februari 14, 2018, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala amesema watumishi hao 18 baadhi yao wamekuwa wakiendelea kujinasibisha kama watumishi wa idara hiyo.

Amesema idara imewatangaza hadharani ili kuisaidia jamii kuwatambua kwamba si watumishi wao hivyo ikitokea miongoni mwao akaendelea kajitambulisha wananchi wachukue hatua ikiwamo kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Watumishi hao ni Thobias Lyewe, Julieth Mrema, Nina Mliga, Loveness Wilson, Wilbard Ompapson, Salama Dilunga, Philbert Chaula, Mkombozi Chodri na Alfred Mrema.

Wengine ni Imakulata Mwakatika, Ramadhani Ally, Ritha Maganga, Jovin Mkuchu, Veronika Max, Angela Mwambwiga, Peter Bally, Elizabeth Kibinga, na Lucy Munyanga.

Akifafanua zaidi, Msemaji wa Uhamiaji, Ally Mtanda amesema “Kuna shida inatokea kwa watu wengi kujitambulisha kuwa wanatoka Uhamiaji. Wanakwenda viwandani na maeneo mengine kisha kuwarubuni watu na kuchukua fedha.”

“Wale kwa namna moja au nyingine walifuzwa kazi na wengine wameacha wenyewe kazi lakini wanaendelea kujitambulisha ndiyo maana tumeamua kuitoa orodha hii ili wananchi wawatambue kwamba hawa si watumishi wetu na hatutahusika kwa lolote likitokea,” amesisitiza Mtanda