Majuto alikuwa tayari kuigiza akiwa kalazwa Muhimbili

Muktasari:

Kauli hiyo imetolewa leo na msanii wa filamu Rehema Abdallah ambaye amekuwa akiigiza na Majuto kama mkewe

Dar es Salaam. Msanii wa filamu, Rehema Abdallah amesema marehemu Amri Athuman maarufu kama Mzee Majuto licha ya kuwa alikuwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alikubali kurekodi sehemu ya filamu akiwa katika hospitali hiyo.

Rehema  ambaye ameigiza na Mzee Majuto tangu mwaka 1978 akicheza mara nyingi kama mkewe, amesema siku chache kabla Majuto hajaanza kumwa alimshauri aanzishe kikundi cha maaigizo Mombasa kutokana na kuwa na mashabiki wengi huko na kuahidi angemsaidia.

Amebainisha kuwa katika mchakato huo alikuwa akimpelekea baadhi ya nyaraka na kuzisaini akiwa MNH na pia alimuahidi atacheza baadhi ya vipande hata kama atakuwa bado amelazwa.

 “Nasikitika hilo la kuigiza na kukamilisha mchakato wa kikundi hicho halijakamilika mzee wetu katutoka, huenda ingekuwa ni kumbukumbu nzuri kwa Watanzania,” amesema.

“Kwani mtu kukubali kucheza hadi akiwa kalazwa hospitali si jambo dogo, ingeacha funzo kwa wasanii namna gani tunatakiwa tuipende kazi yetu bila kujali upo katika hali gani.”

Kuhusu mahali walipokuwa wamefikia katika uanzishwaji wa kundi hilo, Rehema amesema tayari walishapata wasanii 70,  walikuwa katika hatua za mwisho za kuanza kufanya kazi.

Hata hivyo, amesema hajui kama kundi hilo litaweza kuendelea kwa maelezo kuwa mchango wa Mzee Majuto bado ulikuwa ukihitajika kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha uanzishwaji wake.

“Mzee Majuto ndiye alikuwa ananishika mkono na kunielekeza wapi pa kwenda katika kukamilisha masuala mbalimbali yaliyohitajika kwa ajili ya kikundi sasa leo nani atanisaidia kufanya hivyo, yaani sioni tena mwanga mbele wa kulifanikisha hili, namuachia Mungu ndiye aamue,”amesema Rehema.

Mzee Majuto alifariki Agosti 8 mwaka huu akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa Muhimbili na anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwake Kiruku Tanga.