Makaburi yaliyokuwa wazi kwa ajili ya miili ya ajali ya Mv Nyerere yafukiwa

Muktasari:

  • Ajali ya kuzama kivuko cha Mv Nyerere ilitokea mwezi uliopita katika ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 230 na wengine 41 walinusurika.

Mwanza. Makaburi yaliyochimbwa kwa ajili ya kufukia miili ya watu waliofariki dunia katika ajali ya Mv Nyerere yamefukiwa.

Makaburi hayo yamefukiwa juzi ikiwa ni mwezi mmoja tangu ajali hiyo ilipotokea na kusababisha vifo vya watu 230 na wengine 41 kunusurika.

Akizungumza na Mwananchi leo, Mwenyekiti wa mtaa wa Bwisya wilayani Ukerewe, Oru Mageru alisema makaburi hayo yamefukiwa baada ya uongozi wa wilaya kuhakiki kuwa miili yote imeishazikwa.

“Tulisubiri hadi kivuko hicho kinyanyuliwe na baada ya zoezi hilo kukamilika na uongozi kujiridhisha kuwa hakuna mwili wowote mwingine tukalazimika kuyafukia,” alisema Mageru.

Alisema kivuko hicho kwa sasa kimehamishiwa katika ghati ya Kigongo wilayani Misungwi.

Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwisya, Emmanuel Minja amesema wawapoteza wanafunzi 11 kwenye ajali hiyo na miili yao  ilipatikana na kuzikwa.