Makada 431 wa CCM kuwania ubunge Eala

Muktasari:

Makada hao wa CCM jana walipitia na kupendekeza majina ya waliiomba nafasi hizo ambayo yatawasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu kinachotarajiwa kukaa jijini Dar es Salaam leo.

Dodoma. Harakati za kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) zimepamba moto mjini hapa ambapo jumla ya makada 431 kutoka chama kimoja wamejitokeza kuwania nafasi hizo.

Makada hao wa CCM jana walipitia na kupendekeza majina ya waliiomba nafasi hizo ambayo yatawasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu kinachotarajiwa kukaa jijini Dar es Salaam leo.

Akizungumza jana mjini hapa Katibu wa Halmashauri Kuu Organizesheni, Pereila Silima alisema wabunge hao wanapitia sifa za waombaji hao na baadaye watapiga kura za maoni kupendekeza majina ya wagombea wenye sifa zinazotakiwa.

“Kazi kubwa inayofanyika hapa leo ni kupitia sifa za wagombea wote 431 na hatimaye wabunge watapiga kura zao za maoni. Kazi hii si ndogo na huenda tukakesha hapa hadi asubuhi,” alisema.

Silima alisema matokeo ya kura hizo za maoni yanatarajiwa kutumwa jijini Dar es Salaam leo asubuhi ili kamati kuu iweze kuwachuja.

Kwa mujibu wa utaratibu wa CCM, CC itachuja majina ya wagombea 18 ambayo yatapelekwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura na Bunge zima ili wapatikane wabunge sita wataokiwakilisha chama hicho katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala).

“Kamati kuu inatarajia kukutana kesho (leo) mjini Dar es Salaam na matokeo ya kura za maoni zinazopigwa hapa yatatumika kutoa muongozo wa kuwapata makada ambao wanakidhi vigezo vya kuwania nafasi ya kukiwakilisha chama katika Bunge la Afrika Mashariki,” alisema.

Mamia ya makada hao wa CCM jana walikusanyika katika makao makuu ya chama hicho kuanzia majira ya asubuhi huku wengi wakionyesha sura za hofu na shauku kubwa ya kujua hatima yao baada ya mchakato huo muhimu.

Mmoja kati ya makada hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alipoulizwa kwanini wanachama wengi wa chama hicho tawala wamejitokeza kugombania nafasi hizo chache alisema ni kutokana na kushawishiwa na viongozi na wananchi.

“Ah, unajua wakati mwingine tunapata mashinikizo tu kutoka kwa wananchi na viongozi wengine wa juu wa chama kwamba mgombea anafaa kuwa mbunge wa Afrika Mashariki,” alisema kada huyo.