Makada waliosimamia uchaguzi wazua jambo

Muktasari:

  • Suala hilo ambalo Ijumaa lilitolewa ufafanuzi na mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani limeibuka upya huku baadhi ya watu wakichapisha picha za nyakati tofauti, zikiwaonyesha baadhi ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wakiwa katika vazi rasmi la uchaguzi na nyingine katika sare za CCM.

Siku moja baada ya matokeo ya uchaguzi mdogo wa majimbo ya Kinondoni, Siha pamoja na kata tisa kutangazwa, na CCM ikiibuka na ushindi maeneo yote, mjadala umehamia mitandaoni huku suala la baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi kudaiwa kuwa makada wa chama hicho.

Suala hilo ambalo Ijumaa lilitolewa ufafanuzi na mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhani limeibuka upya huku baadhi ya watu wakichapisha picha za nyakati tofauti, zikiwaonyesha baadhi ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wakiwa katika vazi rasmi la uchaguzi na nyingine katika sare za CCM.

Baada ya picha hizo kusambaa watu wanaowajua walianza kuchangia mijadala hiyo kwa namba mbalimbali, baadhi wakisapoti na wengine wakiponda na kuwakejeli.

Kutokana na mjadala huo, mmoja wa makada alilazimika kuondoa kwenye ukurasa wake wa Facebook, picha zake za zamani zinazomwonyesha akiwa kwenye shughuli mbalimbali za chama.

Suala la makada hao lilikuwa moja kati ya hoja sita zilizowasilishwa na viongozi wa Chadema kwa mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, wakihoji kwa nini majina zaidi ya wasimamizi yasiwekwe hadharani ili kama kuna mwenye pingamizi afanye hivyo.

Vilevile, viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walihoji pia uwezekano wa makada hao 3,065 kupiga kura katika vituo wanavyosimamia bila kujiandikisha katika Jimbo la Kinondoni kwa kuwa wanatoka katika wilaya nyingine.

Hata hivyo, katika majibu yake, Kailima alisema taarifa alizonazo taratibu zote zinazohusika kuhusu wasimamizi na wasaidizi wao zilikuwa zimefuatwa.

Kailima alisema, “Kwa taarifa ambazo Tume inazo, taratibu zote za kuwapata watendaji hao zilizingatiwa ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi za kazi, waliohitaji kuomba, kuchujwa waliokuwa na sifa zinazohitajika, kufanyika usaili na majina ya walioteuliwa kuwa wasimamizi kubandikwa kwenye mbao za matangazo katika ofisi za kata zote 10 za Jimbo la Kinondoni.”

Alisema utaratibu huo unaelekezwa na kifungu cha 7(4)(5) 2015 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343, ikisomwa pamoja na Kanuni ya 14 na 15 ya Kanuni cha Uchaguzi za mwaka 2015 na maelekezo kwa wagombea.

Pia alisema kwa mujibu wa barua yenye Kumb. Na. KMC/U21/06/12 ya Februari 11, 2018, msimamizi wa uchaguzi aliwasilisha orodha ya watendaji hao kwenye vyama vinavyoshiriki katika uchaguzi.

Hata hivyo juhudi za kumpata msimamizi huyo jana kufafanua suala hilo hakikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila kupokewa.

Kuhusu madai ya kuwepo kwa wapigakura 3,065 kutokana na watendaji hao ambao wangepiga kura bila kuandikishwa Kinondoni, Kailima alisema hakuna mtu ambaye angeruhusiwa kupiga kura ambaye hajaandikishwa na jina lake halipo katika daftari la wapiga kura.

Alisema utaratibu huo umefafanuliwa na kifungu cha 63(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.