Fahamu umuhimu wa NGOs kiuchumi

Muktasari:

  • Ifahamike kuwa mashirika haya sio ya kibiashara, hivyo hayaanzishwi kwa lengo la kujipatia fedha au faida yoyote zaidi ya kuisaidia jamii husika. Michango inayotolewa na wadau ni lazima ipelekwe katika jamii husika kutatua kero na changamoto mbalimbali. Ili shirika liwe na nguvu kisheria ni lazima lisajiliwe.

Shirika lisilo la kiserikali (NGO) ni shirika la kijamii lenye lengo la kutoa huduma za kijamii kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo. Lengo kuu ni kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo katika jamii. Ifahamike kuwa mashirika haya sio ya kibiashara, hivyo hayaanzishwi kwa lengo la kujipatia fedha au faida yoyote zaidi ya kuisaidia jamii husika. Michango inayotolewa na wadau ni lazima ipelekwe katika jamii husika kutatua kero na changamoto mbalimbali. Ili shirika liwe na nguvu kisheria ni lazima lisajiliwe.

Kwa kawaida wazo la kuanzisha Shirika linaweza kutoka kwa mtu mmoja au kikundi cha watu ambao wanakuwa na maono katika kusaidia na kutatua changamoto walizoziona katika jamii inayowazunguka, baadaye hushirikisha na wengine ambapo kama watakuwa tayari kusaidia kutekeleza maono hayo ndipo huunda kikundi chenye lengo moja na mtazamo mmoja ili kiweze kuhamisha maono kuwa katika mtazamo halisi.

Miongoni mwa wanakikundi hicho ndipo hupatikana viongozi wa kukisimamia kikundi hicho au shirika hilo katika mchakato mzima wa usajili, kuanzia na mapendekezo ya majina ya Shirika, kuandaa vikao vya shirika.

Usajili wa mashirika haya hutofauitiana kulingana na ngazi husika ya utekelezaji wa shughuli za shirika husika.Shirika linaweza likasajiliwa na kufanya kazi katika ngazi ya kata, ambapo katika ngazi hii ofisa mtendaji wa kata husika ndiye atakayehusika na usajili huu kwa kutoa vibali maalumu.

Katika ngazi ya wilaya, mkuu wa wilaya husika ambapo shirika hili litafanya shughuli zake ndiye anayebeba dhamana ya usajili wa shirika hilo. Vilevile katika ngazi ya mkoa, mkuu wa mkoa husika atahusika na usajili wa shirika hilo, lakini katika ngazi ya taifa au kimataifa, Wizara itahusika na usajili wa shirika. Ni lazima ifahamike kuwa kuendesha shirika pasipo kusajiliwa ni kosa kisheria.

Wakati wa usajili wa shirika la namna hii ni muhimu sana mambo yafuatayo yakazingatiwa ili kuweza kukamilisha mchakato wa usajili; Katiba ya shirika nakala 3 zilizofungwa vizuri – ambayo ndani yake kutakuwa na malengo ya shirika, maono ya shirika na mbinu za utekelezaji wa maono hayo. Ndani ya katiba pia itaeleza idadi na aina ya mikutano ya Shirika, muda wa viongozi kukaa madarakani na namna ya mapato na matumizi ya fedha na rasilimali za shirika, namana kutatua migogoro n.k

Wasifu wa viongozi (CV), ifahamike kuwa uimara na uadilifu wa viongozi ndio nguzo imara ya maendeleo na mafanikio ya Shirika, hivyo ni lazima wajumbe wote wa Shirika watafakari kwa kina uwezo wa viongozi wanaowachagua au kuwateua kuliongoza Shirika. Japo wazo la kuanzisha shirika hutoka kwa mtu mmoja mwenye maono lakini si lazima mtoa wazo akawa sehemu ya uongozi. Barua ya utambulisho kutoka ofisi ya mkuu wa Wilaya, barua hii ni muhimu sana katika usajili wa Shirika hasa ngazi ya Kitaifa, barua hii humaanisha kuwa shirika linatambulika kuwepo na kufanya shughuli zake katika Wilaya husika. Barua ya kuomba kusajiliwa kwa Shirika, ni vyema kufahamu kuwa Shirika pia linatakiwa kuwa na barua yake ya kuomba kusajiliwa, na anuani ya barua iendako itategemea na ngazi ya ambayo Shirika linakwenda kusajiliwa. Fomu ya usajili wa shirika (NGO A – Form No.1), hii ni fomu kuhusiana na usajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali. Fomu hii itapaswa kujazwa kikamilifu na kusainiwa na mwenyekiti na katibu wa Shirika husika.

Majina pendekezwa ya shirika yasiyopungua matano na Ada ya Usajili. Majina haya husaidia kutumika kama majina mbadala pale inapotokea baadhi ya majina kufanana na majina ya mashirika mengine yaliokwishasajiliwa au kukataliwa kutokana na sababu nyinginezo za kiutawala na kimaadili). Malipo ya Ada ya usajili ndio kielelezo kuwa mchakato wa usajili umekubaliwa na cheti kinaelekea kutolewa.