Hati ya kiwanja, nyumba fursa ya kukuza uchumi wa kaya

Muktasari:

  • Kwa kuzingatia ukubwa wa eneo wa Tanzania na ukweli kwamba zaidi ya asil-imia 70 ya wananchi wote wanategemea kilimo, urasmishaji wa maeneo haya ni miongoni mwa vitu muhimu ambavyo kila ‘anayetaka mali’ anapaswa kukidhi.

Wahenga walisema kama mnataka mali, mtayapata shambani. Ni msemo unaomaanisha umuhimu wa ardhi kwenye maendeleo ya kiuchumi kwa mwanadamu.

Kwa kuzingatia ukubwa wa eneo wa Tanzania na ukweli kwamba zaidi ya asil-imia 70 ya wananchi wote wanategemea kilimo, urasmishaji wa maeneo haya ni miongoni mwa vitu muhimu ambavyo kila ‘anayetaka mali’ anapaswa kukidhi.

Licha ya wananchi kujitahidi kujenga nyumba za kisasa, za kudumu na zenye vivutio vingi kutosheleza mapumziko ya wamiliki, wengi hawana hati. Nyumba, viwanja na mashamba mengi nchini hay-ana hati.

Takwimu zinaonyesha kuna kampuni 48 za upangaji miji na 42 za upimaji ardhi. Watalaamu wa kampuni hizi wana-takiwa kushirikiana na idara ya ardhi na mipango miji kuhakikisha wananchi hasa wenye kipato cha chini wanarasmishwa.Ulikuwapo mpango wa Mkurabita uli-odhamiria kurasimisha rasilimali za wan-yonge ili kuukimbia umasikini. Mkura-bita ulioanzishwa na kuanza kutekeleza miaka 15 iliyopita, ulikusudia kuongeza thamani ya ardhi, nyumba na majengo tofauti.

Alipokuwa anazungumza na wawakili-shi wa kampuni hizo pamoja na watendaji wa mitaa na vijiji vya kanda ya mashariki, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alizitaka kampuni hizo kuhakikisha wanatoa hati kwenye kila mradi watakaokuwa wanau-tekeleza.Hati hizo, alisema ni njia ya kuwaweze-sha wananchi kiuchumi kwani kuan-zia hapo nyumba, kiwanja au shamba linakuwa na thamani mbele ya taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba.

Mpango huo pia unawahusisha wote waliojenga na wanaoishi kwenye makazi holela. Waziri ameagiza kurasmishwa kwa nyumba zote kwenye maeneo hayo kwa gharama isiyozidi Sh250,000.Urasmishaji huo, pamoja na mambo mengine, unakusudia kuwapa wamiliki uwezi wa kukopa kutoka benki 33 za biashara zinazotoa mikopo ya nyumba ingawa takwimu zinaonyesha uwiano wa wananchi wanaonufaika nayo ni chini ya asilimia moja ya pato la Taifa.

Kuharakisha upimaji, Serikali imeshu-sha mamlaka kutoka wizarani kwenda kwenye ofisi za kanda ambazo zitahu-dumia mikoa yote nchini. Kwa sasa kuna kanda nane zilizopo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mtwara, Moshi, Simiyu, Mwanza, Dodoma na Tabora.

Pamoja na mipango mingine, ofisi hizo zinatakiwa kurahisisha urasmishaji wa makazi holela yaliyopo mjini katika halmashauri zote nchini. Utekelezaji wake uishirikishe sekta binafsi.

“Halmashauri zitoe zabuni kwa kampuni itakayokuwa na gharama ndogo zaidi. Hivi sasa nyingi zinawatoza wananchi kati ya Sh300,000 mpaka Sh850,000 jambo linalowaumiza,” anasema waziri huyu.

Mikopo ya nyumba

Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuna uhaba wa nyumba milioni tatu nchini na kila mwaka kunakuwa na ongezeko la mahitaji ya nyumba 200,000.

Kutokana na ukweli huo, mikopo ya nyumba inakuwa suala muhimu ambalo hata hivyo, Waziri Lukuvi anasema linakabiliwa na changamoto ya waendelezaji wa uhakika.

“Wananchi wengi huwa hawapewi nyumba bali maneno. Nimeiagiza BoT kutoiruhusu benki yoyote kutoa mkopo wa nyumba kabla mteja hajakabidhiwa nyumba,” anasema Lukuvi.

Kwa mujibu wa waziri huyo, wateja wengi wanaonunua nyumba zinazojengwa na taasisi zenye mamlaka hayo nchini hulazimika kusubiri mpaka miaka mitatu kabla ya kukabidhiwa fedha zao jambo linalowaumiza kwani licha ya kukatwa mishahara yao kutokana na mikopo waliyochukua benki, hulazimika kulipa kodi ya nyumba.

“Kuanzia sasa, nataka kampuni ziuze nyumba. Si mwananchi anakatwa na benki na bado analipa kodi kwenye nyumba aliyopanga,” anasisitiza.

Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC) huzikopesha benki za biashara ili nazo ziwakopeshe wananchi ili kuharakisha uboreshaji wa makazi nchini.

Pamoja na jukumu hilo, changamoto iliyopo ni uchache wa wananchi wenye hati za ama maeneo wanayoyamiliki au nyumba walizonazo suala linalosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mmoja wa maofisa wa TMRC aliyekuwa anatoa elimu kwenye maonyesho ya Sabasaba yaliyokamilika mwishoni mwa wiki iliyopita, anasema kwa wananchi wenye hati, hawapati usumbufu wowote kupata mkopo.

“Ukiwa na hati mbona utagombewa. Kila benki itataka kukukopesha,” anasema ofisa huyo ambaye si msemaji wa TMRC.

Kumbukumbu zinaonyesha kampuni hiyo yenye benki wanachama 33 ina zaidi ya Sh54 bilioni ilizokopeshwa na Benki ya Dunia ambazo zinapaswa kukopeshwa mpaka Juni mwakani.

Kufanikiwa kupata mkopo wa ama kujenga, kununua au kukarabati nyumba, mteja anahitaji kuwa na hati ya kiwanja au nyumba anayotaka kuinunua au kuikarabati.

Uratibu

Kuhakikisha wananchi wengi wanapata hati kutoka kwa kampuni binafsi zitakazoshirikiana na maofisa wa idara ya ardhi na mipango, kuanzia Julai Mosi halmashauri ndizo zinatakiwa kuratibu shughuli zote za upimaji, uendelezaji na urasmishaji wa maeneo badala ya mitaa kama ilivyokuwa zamani.

Utaratibu utakaotumika ni kila mtaa au kijiji kuwasilisha mahitaji yake halmashauri ambayo itapokea na kutangaza zabuni ya upimaji kwa kampuni binafsi kulingana na mipango iliyopo.

“Licha ya upimaji, halmashauri izungumze na kampuni husika kuweka gharama ya hati. Upimaji wowote utakaofanywa kuanzia Julai Mosi ni lazima umpe mwananchi hati yake,” anaaagiza waziri huyo.

Kuongeza hamasa kwa wananchi kurasmisha maeneo yao, Serikali imetangaza kupunguza tozo ya hati kutoka asilimia 2.5 mpaka asilimia moja. Punguzo litakalowahusu wanaotaka kurasmisha makazi yao hasa waishio kwenye makazi holela.

“Serikali inawatambua wananchi masikini hawana uwezo wa kuwafikiwa maofisa ardhi. Hawa wamepunguziwa ili nao wasiikose fursa ya kumiliko hati ya nyumba,” anasema.

Vifaa vya upimaji

Miongoni mwa vitu vinavyoongeza gharama za upimaji na upangaji miji ni vifaa vinavyotumika kufanikisha suala hilo. Kampuni nyingi binafsi, hulazimika kukodi baadhi kutokana na kutokuwa navyo vyote.

Gharama hizo huwarudisha nyuma baadhi ya wahitimu wa fani husika wenye uwezo wa kuanzisha kampuni na kusaidia kufanikisha upimaji na upangaji miji.

Kwa kulitambua hilo, Serikali imeandaa utaratibu wa kuwawezesha ili washiriki kupima na kupanga hivyo kuboresha makazi nchini.

Kufanikisha hilo, waziri anasema Serikali imeagiza vifaa vyote muhimu vinavyohitajika ambavyo vitasambazwa kwenye halmashauri ambako kampuni za upimaji na upangaji miji zitaweza kukodi kutekeleza majukumu yaliyopo.

“Tunataka mchanganuo wa gharama za kukodi vifaa hivyo uonyeshwe kwenye taarifa za kampuni ambazo zitatakiwa kuanza kulipa kodi ya Serikali,” anakumbusha Lukuvi.

Wadau

Mhandiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Omari Mbura anasema ipo haja ya kuboresha uhusiano kati ya mashirika yanayojenga nyumba na TMRC.

“Mashirika haya ni wadau muhimu kwa TMRC. Endapo utaratibu rafiki utaandaliwa, yanaweza kukopeshwa kwa kutumia mali zao kama dhamana ya mikopo kufanikisha utekelezaji wa miradi waliyonayo kabla ya kuuza nyumba kwa wananchi,” anashauri Dk Mbura.

Anasema kurahisishwa kwa upimaji na upatikanaji wa hati utawahamasisha wananchi wengi kupima maeneo yao hivyo kukidhi vigezo vya kukopesheka mikopo ya nyumba.

Pamoja na ukweli huo, anashauri kuongezwa kwa kasi ya ujenzi wa nyumba kuendana na ile ya ongezeko la watu ili kupunguza uhaba uliopo.

Mtaalamu wa masuala ya benki na mikopo ya nyumba, Asanterabi Lotha anasema kuna mambo mengi yanapaswa kufanyiwa kazi na wadau wote wa sekta ya nyumba nchini ili kuongeza ufanisi unaohitajika.

“Anazishauri benki kutafuta vyanzo vya mapato ya muda mrefu huku Serikali ikijitahidi kudhibiti riba wanayotozwa wakopaji ambayo inafika mpaka asilimia 18,” anasema Lotha.

Licha ya riba, anaitaka Serikali kutoa elimu zaidi kwani wananchi wengi bado wanaamini upatikanaji wa hati, sifa inayohitajika kukopesheka, ni mchakato unaochukua siku nyingi sana.

Kwenye upimaji pia, anashauri halmashauri ziwape hamasa wananchi kupima maeneo yao kwa bei zinazoeleweka, mchakato uwe wa wazi.

“Wapo baadhi ya wananchi wanaamini mikopo ni suala baya. Hawa wanahitaji elimu, jamii ishiriki kuwatoa kwenye uelekeo huo,” anasema mtaalamu huyo.