Huwa unazingatia nini kabla ya kufanya mkataba?

Muktasari:

Tunatekeleza wajibu huo, yapo mambo ya msingi tunayopaswa kuyazingatia. Kwanza, miongonimwa mambo hayo ni kuangalia uhalali wa mkataba husika.

Mara nyingi, kwa sababu moja au nyingine, huwa tunalazimika kufanya mikataba ya aina tofauti kulingana na mahitaji yaliyopo.

Tunatekeleza wajibu huo, yapo mambo ya msingi tunayopaswa kuyazingatia. Kwanza, miongonimwa mambo hayo ni kuangalia uhalali wa mkataba husika.

Watu wengi wamejikuta wameingia kwenye makubaliano ambayo wenyewe huita mkataba lakini ukiichunguza kisheria, ni makubaliano tu ya aina fulani ambayo hayana nguvu yoyote kisheria.

Ili makubaliano yoyote unayoyafanya juu ya jambo lolote yawe na nguvu kisheria ni lazima yawe na nia ya kuwajibika, malipo halali, uwezo au mamlaka ya kuingia katika mkataba, uhiyari na uhalali wa jambo ambalo mmekubaliana.

Usiingie katika mkataba wowote kama mambo hayo yote matano hayapo. Kukosekana kwa jambo mojawapo kati ya hayo kunaondoa uhalali wa mkataba au makubaliano hayo.

Kitu kingine ni kutomuamini mtu kupita kiasi. Wengi wamefanya makubaliano ya maneno na mzazi, ndugu, muumini mwenzake, kiongoni wa dini, mwalimu, bosi au mfanyakazi mwenzake na mwisho wakaishia kujuta kwa uaminifu walioutoa.

Mwenye tatizo hapo hakuwa aliyemtenda bali aliyetendwa. unayemwamini mtu kupita kiasi wakati hakuna binadamu anayepaswa kuaminiwa kwa kiasi hicho duniani hasa kwenyemali au fedha ndiwe mwenye tatizo.

Tatizo lako hukutengeneza mazingira ya kuwajibika kisheria, ndiyo maana ikawa rahisi kulizwa.

Hata baada ya kuweka mazingira ya kuwajibika, unapaswa kuhakikisha mkataba upo kwenye maandishi. Usiingie kwenye makubaliano ya maneno kwani utakuja kushangazwa utakapogeukwa na mtu unayemuamini.

Kama umeajiriwa, hakikisha una mkataba wa kazi, kama umemkopesha mtu fedha basi unao mkataba bila kujali kiwango cha fedha na ukinunua kitu pia kuwe na mkataba kati ya muuzaji na mnunuzi au risiti itakayothibitisha muamala husika.

Kama umeoa usisahau kumshirikisha mwenza wako. Jambo la msingi katika mikataba hasa unapoingia na taasisi, jumuia, jamii, kanisa, msikiti, kikundi au familia ni muhimu ukawashirikisha wahusika wakuu au wadau wa taasisi hiyo ili watoe maoni yao kabla hamjakubaliana.

Usiingie mkataba kwa pupa. Ni vyema kusubiri kidogo kuliko kukosa baraka za wengine ambazo ni muhimu kisheria. Hata kama wewe ndiye mkurugenzi mkuu, au baba wa familia usithubutu kufanya uamuzi utakaoathiri mustakabali wa taasisi au familia bila wahusika wakuu kuwa na taarifa.

Kutokana na kuathiriwa na mfumo dume wanaume wengi hufanya uamuzi mkubwa unaoathiri hatma ya familia bila kumshirikisha mke au watoto na matokeo yake kusababisha usumbufu mkubwa. Usithubutu kufanya hivyo.

Ikihitajika, muone mwanasheria ambaye ni muhimu kukusaidia kuuandaa na kukushauri kabla hujaingia katika mkataba huo. Unaweza ukafikiri unapunguza gharama kwa kufanya mikataba kienyeji lakini hasara utakayopata baadaye yaweza kuwa kubwa zaidi ya ambayo ulidhani umeiokoa.

Hakikisha mkataba wako umesainiwa na kugongwa muhuri na mwanasheria kwa sababu huyo atakuwa msaada kwako endapo mwenzako atavunja au hataheshimu vipengele vya mkataba huo.

Usisubiri mambo yakuharibikie ndipo uanze kutafuta msaada wa kisheria. Ni vyema ukachukua tahadhari kabla ya hatari. Japokuwa wakati mwingine kinga huwa na gharama ila ni bora kwani itakulinda katika hali zote za mikataba yako kuliko kusubiri usumbufu utakaoupata wakati unatafuta hukumu ya kisheria.