Jua namna bora ya kuandaa chakula cha mifugo

Jinsi ya kuandaa chakula cha mifugo.

Muktasari:

Hata hivyo, changamoto kubwa wanayokumbana nayo wafugaji wengi ni gharama kubwa ya vyakula vya mifugo, jambo wanalosema limekuwa likiwaingiza katika hasara.

Sifa za utengenezaji wa chakula cha mifugo ni pamoja na mhusika kuwa na elimu ya lishe kwa mifugo na kujua virutubisho vinavyotakiwa kwa mifugo.

Mwamko wa kufuga umetamalaki kwa Watanzania wengi. Vijijini hata mijini, wananchi wanajihimu kuendesha miradi mbalimbali ya ufugaji hasa ule wa kuku ambao umekuwa kimbilio la walio wengi.

Hata hivyo, changamoto kubwa wanayokumbana nayo wafugaji wengi ni gharama kubwa ya vyakula vya mifugo, jambo wanalosema limekuwa likiwaingiza katika hasara.

Kwa mfano, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika siku za karibuni, umebaini kuwa bei ya chakula cha kuku wa nyama na mayai aina ya ‘Starter’ huuzwa kuanzia Sh60,000 kwa mfuko wa kilo 50.

Aina nyingine za chakula kama ‘Grower na Finisher zinauzwa kwa bei ya Sh40,000 na Sh50,000 mtawalia. Kwa wafugaji wadogo na wale wanaoanza, gharama hizi ni kubwa.

Kama njia ya kuondokana na changamoto hii, baadhi ya wafugaji wameamua kutengeneza vyakula kwa kutumia malighafi mbalimbali kama inavyoshauriwa na wataalamu. Lakini pia wapo wanaotengeneza vyakula hivyo kienyeji, hivyo kuathiri afya na ubora wa mifugo yao.

TAFMA yajitosa kuwasaidia wafugaji

Kuwepo kwa wafugaji wanaoandaa vyakula kimakosa, kumeifanya Jumuiya ya wazalishaji wa vyakula vya mifugo Tanzania (TAFMA), iwe inaandaa mafunzo kwa ajili ya kufundisha namna bora ya uchanganyaji wa vyakula vya mifugo.

Katibu wa jumuiya hiyo, Sufian Kyarua, anasema semina hizo hufanyika kutokana na kutambua kuwa katika utengenezaji wa chakula wafugaji wengi, wamekuwa wakitumia malighafi zisizofaa au zenye kiwango duni cha ubora, hivyo kupata hasara.

Anasema kimisngi, uzuri wa chakula, hutokana na ubora wa malighafi iliyotumika kuanzia katika uvunaji na namna ilivyohifadhiwa.

“Baadhi ya malighafi zinapochelewa kuvunwa au zilizovunwa kwa muda muafaka na kuhifadhiwa sehemu yenye unyevu, huwa zinatengeneza sumu kuvu ambayo hukinzana na ukuaji wa mifugo,” anaeleza.

Anaongeza: “Mtu anaweza kutumia pumba ambayo ilikobolewa kwa mfumo wa kutumia maji ili mahindi yakoboke vizuri, lakini baada ya hapo pumba inawezekana hazikuanikwa vizuri zikavunda, hivyo sumu kuvu inakuwa tayari ipo na endapo zitatumika kama chakula, zitaleta madhara kwa mifugo.’’

Pia anasema ubora wa malighafi wa sehemu moja hutofautiana na ule wa sehemu nyingine kulingana na rutuba ya udongo pamoja hali ya hewa.

Akifafanua hili, anasema:“Mahindi yanayolimwa Tanga yanaweza kutofautiana katika kiwango cha wanga na protini ikilinganishwa na yale yanayotoka Rukwa au Dodoma. Unapotengeneza chakula, lazima uzingatie madini yanayopatikana.’’

Anasema wafugaji wengi pia wamekuwa hawajui watumie kanuni gani katika kutengeneza chakula cha mifugo yao. Wengine anasema hutengeneza kanuni ambayo haiendani na aina ya mifugo waliyoikusudia jambo linaloathiri ukuaji wao.

“Mifugo ina mahitaji tofauti; ukimpa mnyama chakula ambacho hakiendani naye, uzalishaji utashuka. Kama ni kuku wa mayai atakuwa hatagi kwa kiwango kinachotakiwa; kama ni kuku wa nyama atashindwa kukua katika muda uliotarajiwa,” anasema Kyarua.

Njia bora za utengenezaji chakula

Anasema ili mfugaji aweze kutengeneza chakula kizuri kwa ajili ya mifugo yake, lazima atumie malighafi bora, awe na taaluma ya lishe ya wanyama ili kujua mnyama anayemtengenezea chakula anahitaji nini na kutambua virutubisho vinavyotakiwa.

“Ukishajua anahitaji nini utajua virutubisho hivyo vinapatikana katika malighafi gani na vimehifadhiwa katika sehemu inayostahili na hapo ndipo utatumia kanuni kujua uchanganye nini na nini kwa viwango unavyohitaji,” anasema Kyarua.

Baada ya kufanya uzalishaji, mfugaji anashauriwa kwenda kupima chakula maabara ili kujua utapata virutubisho vya aina gani na kama amefikia kile anachokihitaji. “Kila sampuli moja inapimwa kwa Sh20,000 hadi Sh25,000 na inaweka urahisi kwako kujua chakula hicho kinafaa kwa mfugo wa umri gani,” anaongeza kusema.

Uchanganyaji chakula cha mifugo

Uchanganyaji wa chakula ni maarifa yanayomwezesha mzalishaji kutengeneza chakula chenye virutubisho vinavyohitajiwa na miili ya wanyama mbalimbali katika ukuaji wao na uzalishaji.

Kwa mujibu wa Kyarua, kuna aina mbili za uchanganyaji wa chakula ambazo ni njia ya kisasa na ya kienyeji. Kwa njia ya kisasa, malighafi husagwa kwa viwango vilivyoshauriwa ili kufikia mchanganyiko ambao utakua na virutubisho vilivyokusudiwa.

“Kuna mashine za kisasa zinazofanya kazi hiyo, lakini kuna njia ya kienyeji ambayo hutumiwa na watu wenye kuku wachache. Hawa hutwanga chakula na kuchanganya kulingana na mahitaji yao,” anaeleza.

Miongoni mwa malighafi zinazotumika katika utengenezaji wa chakula cha mifugo ni mahindi, mtama, muhogo kwa ajili ya kutengeneza wanga.

Pia kuna mashudu ya soya, dagaa, pumba za mahindi na ngano, madini ya chokaa, vitamin na vichanganyio vingine kutoka viwandani ambavyo ni ‘premixes’ na ‘limestone’, ‘bone meal’,’ MCP’,’DCP’.

Tofauti ya vyakula

Anasema tofauti kubwa ya ubora wa chakula kinachotengenezwa na wafugaji wa kawaida na kile kinachotengenezwa viwandani ni utaalamu na utumiaji wa malighafi. “Watu wanaojishughulisha na utengenezaji wa chakula, wanakuwa na wataalamu wenye elimu ya lishe ya mifugo, vifaa, wanatumia maabara kuthibitisha ubora wa malighafi na wanajua ni chakula kipi kinafaa kwa kila aina ya mifugo,” anasema.

Lakini kwa walio wengi anasema ama wanakosa uelewa wa mbinu bora za ufugaji au kukosa mitaji kwa ajili ya kuandaa mazingira bora ya afya za mifugo yao.

“Wengi hawana taaluma ya lishe ya chakula hivyo inakuwa ni ngumu kutengeneza chakula kwa ajili ya mifugo yao. Uhifadhi wa malighafi pia unashusha viwango vya utengenezaji wa vyakula vya mifugo yao,” anaeleza.

Faida za kutumia vyakula bora

Kwa mujibu wa Kyarua, kuna faida kadhaa kama mfugaji atazingatia kanuni bora za ulishaji wa mifugo, ikiwamo matumizi madogo ya madawa, hivyo kuwa na uhakika wa kuzalisha mifugo iliyo salama kwa afya za walaji.

Anasema kuwa mnyama anayetumia dawa mara kwa mara, hudumaa katika ukuaji wake na faida zinazopatikana huwa ndogo ikilinganishwa na yule asiyetibiwa mara kwa mara.

“Gharama za uzalishaji zikipungua atafanikiwa kuongeza faida katika biashara yake na atamhakikishia mlaji kuwa bidhaa anazozalisha ni salama, kwa sababu hazitegemei madawa katika ukuaji,”